Yanga yaombewa dua

Image caption Rais wa Shirikisho la soka Tanzania Jamal Malinzi.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania ( TFF) , Jamal Malinzi ameitakia kila la kheri timu ya Young Africans katika mchezo wake wa Jumamosi wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CC) dhidi ya timu ya Etoile du Sahel kutoka Tunisia, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi, saa tisa jioni kwa saa za Afrika ya Mashariki

Katika salamu zake kwa klabu ya Young Africans, Rais Malinzi amewaambia wanapaswa kupambana na kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano kwani ndio pekee kwa sasa wanaoipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Young Africans imeingia katika hatua ya 16 bora Kombe l Shirikisho barani Afrika,baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao (3-2), kisha kuwaondoa FC Platinum ya Zimbabwe katika hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao (5-2).

Endapo timu ya Young Africans itafanikiwa kuwaondoa Etoile du Sahel itasuburia kucheza mechi ya mtoano (Play-off) dhidi ya timu mojawapo zitakaotolewa katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CL).