Stars kukwaana na Mapharao wa Misri

Image caption Wachezaji wa timu ya Taifa stars wa Tanzania, wakishangilia.

Katika kile kinachoonekana kujiandaa na kibarua kigumu dhidi ya Mapharao wa Misri, timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ina mpango wa kuweka kambi nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na mechi ya kufuzu kucheza fainali za kombe la Mataifa barani Afrika za mwaka 2017 (AFCON)zitakazofanyika nchini Gabon.

Stars imeapangwa katika kundi la “kifo” dhidi ya Misri, Nigeria na Chad kwa ajili ya kutafuta timu mbili zitakazofuzu kutoka katika hilo. Mechi ya kwanza kati ya Taifa Stars na Misri itachezwa hapo Juni 13.

Ugumu wa Stars kupenya katika tundu la sindano ni kutokana na viwango vya timu pinzani, Nigeria ipo nafasi ya 45 katika viwango vya FIFA na Misri ipo nafasi ya 5. Ikiwa chini ya kocha Mdachi, Mart Nooij, Stars ipo nafasi ya 107 na katika kundi lao la G, Chad ndio timu iliyo chini katika viwango hivyo, ikiwa nafasi ya 151.

Raisi wa Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema huenda Stars ikaweka kambi nchini Ethiopia ili kujiandaa na mechi hiyo.

Malinzi amesema timu hiyo inaweza kuushangaza ulimwengu kwa kufuzu na kuzitoa timu hizo zenye uzoefu wa mikiki mikiki ya michuano ya Afrika na ile ya kombe la dunia.