Tanzania kuongeza makocha timu ya ngumi

Shirikisho la ngumi nchini Tanzania (BFT) lina mpango wa kuongeza makocha watatu katika kambi ya timu ya taifa kwa ajili ya kumsaidia kocha mkuu, Benjamin Mwangata kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya kujiiandaa na Michezo ya Afrika itakayofanyika nchini Congo Brazzaville kuanzia Septemba 4-19 mwaka huu.

Katibu mkuu wa BFT, Makore Mashaga amesema kuwa makocha watakaoongezwa watasaidia sana katika maandalizi ya timu hiyo.

“Ni kawaida kwa timu ya ngumi kuwa na makocha wengi, kwa sababu wapo ambao watatoa mafunzo ya vitendo na wengine kutoa maelekezo”, amesema Mashaga.“Tuna imani na mabondia wetu watafanya vizuri, hivyo tunataka kuwapa mazoezi ya uhakika”.

Tayari BFT imeweka mkakati wa kushiriki michuano ya kimataifa kama sehemu ya maandalizi nchini Zambia na Serbia mwezi May na July.

Mabondia wa Tanzania kwa sasa wanafanya mazoezi katika uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi.

Mabondia hao ni Mohamed Mzeru, Maulid Athumani, Ibrahim Abdalah (uzito wa light- fly), Juma Ramadhani, Said Hofu, (uzito wa fly), Ahamad Furahisha, Bon Mlingwa, Elias Mkomwa, Bosco Bakari (uzito wa bantam).,