Simba kuwalipa wachezaji wake wa zamani?

Image caption Kikosi cha Simba

Klabu ya Simba SC imetakiwa kuwalipa wachezaji wake wawili wa zamani akiwemo mchezaji wa kulipwa, Amisi Tambwe kutoka Burundi mamilioni ya shilingi za Kitanzania kutokana na kuvunja mikataba yao ya kazi, au vinginevyo Shirikisho la soka (TFF) litachukua sshemu ya mapato ya klabu hiyo kutoka katika mgao wake wa viingilio vya mechi za ligi kuu ili kuwalipa.

TFF, kupitia kamati yake ya Sheria na Hadhi za wachezaji, imeitaka Simba kumlipa mchezaji Haruna Chanongo sh. 11,400,000 ( dola zipatazo 5,500 ) kufikia Ijumaa (April 30, 2015) vinginevyo Sekretarieti ya TFF itaanza kukata mapato ya Simba ili kumlipa mchezaji huyo.

Kamati hiyo pia imewaamuru mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara ambao wameiwakilisha nchi katika michuano mbalimbali ya CAF yaliyopita kumlipa mchezaji wake wa zamani, Amissi Tambwe kutoka Burundi pesa zipatazo milioni 14.

Tambwe,mfungaji bora wa msimu uliopita (akiwa Simba) ambaye kwa sasa anachezea klabu pinzani ya Yanga, aliwasilisha malalamiko dhidi ya Simba ya kutolipwa dola 7,000 za Marekani zilizotokana na klabu hiyo kuvunja mkataba wake Desemba 15, 2014. Uamuzi wa kuvunja mkataba ulikuwa ni wa makubaliano ya pande zote ambapo Simba ilitakiwa iwe imemlipa fedha hizo mlalamikaji kufikia Desemba 17, 2014.

Kwa mujibu wa Afisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, katibu Mkuu wa Simba SC , Steven Ally alikiri klabu yake kudaiwa na mchezaji huyo na kuwa wameshafanya mawasiliano na wakili wake aliyepo Ureno, Felix Majani na kupanga utaratibu wa kumlipa isipokuwa kilichokuwa kinasubiriwa ni kusaini hati ya makubaliano ya malipo (Deed of Settlement).

Kizuguto amesema kamati imesikitishwa na klabu ya Simba kushindwa kumlipa mchezaji huyo kama ilivyokuwa katika makubaliano ya kuvunja mkataba yaliyofikiwa na pande zote mbili Desemba 15, 2014.

Image caption Je Simba itawalipa wachezaji hao wa zamani?

Kufuatia kushindwa kumlipa ndani ya makubaliano, Klabu ya Simba inatakiwa kumlipa Amissi Tambwe fedha hizo kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ya dola 5,000 malipo yawe yamefanyika kufikia Ijumaa ( Aprili 30, 2015).

Salio la dola 2,000 ili kukamilisha jumla ya dola 7,000 liwe limelipwa kufikia Mei 10, 2015, uamuzi ambao upande wa Simba ulikubaliana nao.

Wakati huo huo, klabu ya Ndanda SC imeamuriwa kumlipa mchezaji Amiri S. Msumi kiasi cha fedha sh. 2,600,000 ikiwa ni pesa yake ya kukubali kuichezea klabu hiyo (signing fee).