Simon Msuva atorokea Afrika ya Kusini

Image caption Simon Msuva

Mfungaji bora wa ligi kuu Tanzania Bara, Simon Msuva ameripotiwa kuitoroka klabu yake ya Yanga na kuelekea afrika ya Kusini kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Orlando Pirates.

Msuva, winga wa Yanga ambaye ameiwezesha klabu yake kuwa mabingwa wa ligi hiyo katika msimu huu, ndiye mfungaji anayeongoza kwa sasa katika ligi hiyo inayotegemewa kufikia tamati siku chache zijazo akifuatiwa na Mrundi Amisi Tambwe mwenye magoli 14, aliomba ruhusa kwa uongozi wa Yanga kwenda bondeni kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa lakini uongozi wa timu ulimkatalia na kumuomba asubiri mpaka ligi itakapoisha , lakini leo amepanda ndege kwenda Johannesburg.

Afisa mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amesema wamesikia taarifa za Msuva kuondoka na kama ni kweli atakuwa amefanya makosa.

Tangu ajiunge na Yanga SC mwaka 2012 akitokea Moro United, Msuva ameifungia timu hiyo mabao 35 jumla katika mechi 102 za mashindano yote.