Amisi Tambwe ajivunia soka la Tanzania

Image caption Amisi Tambwe akiwa na mpira aliopewa baada ya kufunga hat trick

Mshambuliaji wa kimataifa wa klabu ya Yanga kutoka nchini Burundi, Amisi Tambwe amesema anajivunia mafanikio aliyoyapata baada ya kuiwezesha timu yake kutwa ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara kwa msimu wa mwaka 2014/2015.

Tambwe amekuwa katika nafasi ya pili ya ufungaji bora msimu huu akiwa na mabao 14, huku mchezaji mwenzake, Simon Msuva akiwa kinara wa ufungaji kwa jumla ya magoli 17.

“Nimejisikia furaha kuiwezesha Yanga kuwa mabingwa, ni mafanikio katika klabu na mchezaji pia”, amesema Tambwe.

Tambwe amekuwa na sifa ya ufungaji magoli nchini Tanzania kwa kutumia kichwa anapopata nafasi hasa kupitia mipira ya kona au ya juu inayoelekea golini.

Katika msimu wa ligi uliopita, Tambwe ndiye aliyekuwa mfungaji bora wakati huo akiichezea timu ya Simba, ambayo msimu huu imemaliza nafasi ya tatu, huku Azam (waliokuwa mabingwa watetezi) ikiwa nafasi ya pili.