Klabu Tanzania Bara zapongezwa

Image caption Kikosi cha watoto wa Jangwani,Yanga.

Chama cha soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimezipongeza klabu za Yanga, Azam na Simba kwa kumaliza katika nafasi za juu kwenye ligi kuu Tanzania bara, iliyomalizika jumamosi mei 9,2015.

Yanga ambao wameibuka mabingwa, Azam wakiwa washindi wa pili na Simba wa tatu zipo katika mkoa wa Dar es Salaam. Kutokana na hoja hiyo, kamati ya utendaji ya DRFA chini ya mwenyekiti wake Almas Kasongo,imesema ni jambo la kufurahisha kuona timu hizo zimefanya vizuri kisoka na kuwa mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine. Ligi hiyo inahusisha timu kutoka mikoa mbalimbali.

Timu hizo zimepongezwa kutokana na matayarisho waliyoyafanya tangu kuanza kwa msimu,ambapo mabenchi ya ufundi yameonesha kuwa na nia ya dhati kuleta ushindani katika ligi.

Yanga SC na Azam Fc ndizo zitakazoiwakilisha nchi katika michuano ya vilabu barani Afrika,ambapo Yanga itakwenda huko kuwania kombe la klabu bingwa baada ya kutwaa uchampioni,huku Azam ikiwania kombe la shirikisho baada kumaliza katika nafasi ya pili, wakati Simba imemaliza katika nafasi ya tatu.