Michuano ya COSAFA yaanza Africa Kusini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Michuano ya COSAFA,nchini Afrika Kusini

Michuano ya kumi na tano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu kusini mwa Afrika,COSAFA imezikutanisha timu za ukanda huo nchini Afrika Kusini. Michuano hiyo ilianza kutimua vumbi Jumapili mei 17 na itakamilika mei 30

Timu 12 kati ya 14 kutoka nchi wanachama wa COSAFA tayari zipo nchini Afrika Kusini kuchuana katika mashindano hayo. Angola na Comoro ambazo ni wanachama wa COSAFA hazikuweza kushiriki mwaka huu.

Nafasi zao zimechukuliwa na Ghana iliyofikia fainali za michuano ya Caf ya mwaka huu na Tanzania kutoka ukanda wa Afrika mashariki na kati ikiwa mwanachama wa CECAFA.

Timu nane zenye viwango vya chini kwa ubora kwa mujibu wa takwimu za FIFA kwa mwezi Februari, zimepangwa katika makundi mawili yenye timu nne kila moja, Tanzania ikiwemo katika michuano hiyo.

Kundi A lina timu za Zimbabwe, Namibia, Seychelles na Mauritius. Ambapo kundi B lina timu za Madagascar, Lesotho, Swaziland na Tanzania.

Katika kundi A Zimbabwe inaoongoza kundi hilo kwa kujikusanyia pointi sita baada ya michezo miwili ikifuatiwa na Namibia yenye pointi nne. Seychelles ni ya tatu na pointi moja. Mkiani ni Mauritius ambayo haina pointi.

Na katika kundi B, Madagascar na Swaziland zote zina pointi tatu, huku Lesotho na Tanzania zikiwa mikono mitupu.

Tanzania leo,Jumatano inarusha karata yake ya pili kwa kupambana na Madagascar baada ya kucharazwa bao 1-0 na Swaziland katika mchezo wake wa kwanza.

Timu za juu katika kila kundi zitasonga mbele hatua ya mtoano, ambapo timu sita za viwango vya juu zitaingia katika mashindano hayo yakiwa katika hatua ya robo fainali na kuendelea. Afrika Kusini kutokana na ubora wake itapambana na Botswana hatua ya robo fainali.