Blatter azungumzia kashfa ya rushwa,Fifa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Askari wakiwakamata baadhi ya viongozi wa Fifa wanaotuhumiwa kwa rushwa

Rais wa FIFA Sepp Blatter ameibuka na kuzungumzia kashafa ya rushwa ndani ya shirikisho hilo kwa kusema wale wao watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo hawana tena ndani ya shirikisho hilo la Soka Duniani.

Maoni yake yamekuja,huku idara ya sheria ya Marekani ikisema kuwa kushikiliwa kwa baadhi ya viongozi hao wa Fifa kunafuatia matokeo ya uchunguzi wa miaka 20 ya mienendo ya rushwa ndani ya shirikisho hilo..

Hata hivyo kwa mjibu wa uchunguzi wa vitendo hivyo vya rushwa ndani ya Fifa umebainisha kuwa viongozi hao wanatuhumiwa kuhusishwa na rushwa ya kiasi cha dola million 150 ndani ya kipindi cha miaka 20.

Awali idara ya sheria ilieleza kuwa viongozi hao wa Fifa wanaotuhumiwa ni 14 wakiwemo tisa ambao wanaendelea na uongozi na wengine ni wale waliomaliza muda wao ndani ya shirikisho hilo la Fifa.

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza ni kwa vipi Blatter amekuwa Kiongozi wa Fifa kwa muda mrefu namnahiyo , pamoja na kuwepo kwa ripoti nyingi za vitendo vya rushwa lakini ameendelea kushikilia wadhifa huo.

Wizara ya sheria ya Uswiss imesema katika tamko lake siku ya jumatano kuwa maafisa wa serikali ya Marekani waliwashuku maafisa hao kupokea rushwa ya dola milioni 100, tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 kwa ajili ya michuano ya Amerika ya kati.

Serikali ya Uswiss imesema itaidhinisha haraka kusafirishwa kwao.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Blatter alisema anafahamu baadhi ya wafanyakazi wenzake wa zamani walikuwa wakichunguzwa lakini amekanusha kuwa uchunguzi huo ulimhusu pia.