Hofu Russia na Qatar kupokonywa uwenyeji

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Hofu Russia na Qatar kupokonywa uwenyeji wa kombe la dunia

Hofu imetanda Russia na Qatar huenda zikapokonywa uwenyeji wa kombe la dunia 2018 na 2022 iwapo ushahidi wa ufisadi utapatikana dhidi yao.

Afisa wa FIFA Domenico Scala ameiambia jarida moja la Uswisi, Sonntagszeitung, kuwa haki ya kuandaa mashindano hayo ya dunia itakuwa katika hatari kubwa iwapo kutaibuka ushahidi wa kutosha kuwa mataifa hayo mawili yalitoa rushwa.

Hata hivyo Scala amekanusha kuwa hadi sasa amepata wala kuona ushahidi wa aina yeyote dhidi ya mataifa hayo mawili.

Scala ambaye anahudumu kama kiongozi wa kamati ya uhasibu na uchunguzi

''iwapo ushahidi utatokea kuwa uteuzi wa mataifa hayo mawili haukuwa wa kweli na haki bila shaka watapokonywa uwenyeji wa mashindano hayo''

"hadi kufikia leo hakuna ushahidi wa kutosha wa kulazimisha hatua kuchukuliwa.''

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hofu Russia na Qatar kupokonywa uwenyeji wa kombe la dunia

Hii si mara ya kwanza kwa Scala kutoa onyo hilo.

Mwaka wa 2013 Scala alitoa onyo hilo japo sasa inatoa maana mpya hususan baada ya kuibuka wimbi la madai ya rushwa na ufisadi katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita.

Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Sepp Blatter alisema kuwa atajiuzulu kama rais wa shirikisho hilo kufuatia kashfa ya ufisadi.

Blatter alichaguliwa tena wiki iliyopita licha ya maafisa wake saba wakuu kukamatwa siku mbili kabla ya uchaguzi .

Lakini alisema kuwa utawala wake hauungwi mkono na kila mtu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Urusi alipopokea rasmi ithibati ya kuandaa makala yajayo ya kombe la dunia

FIFA inakumbwa na mgogoro wa kukamatwa kwa maafisa wake kutokana na mashtaka ya ufisadi ikiwa ni miongoni mwa mashtaka yaliofunguliwa na Marekani .

Uchunguzi mwengine unaofanywa na serikali ya Switzerland kuhusu vile michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2018 na 2022 ilitolewa pia unaendelea.

''Nimehusika sana na FIFA na maslahi yake.''

''Kilicho muhimu kwangu ni taasisi ya FIFA na soka duniani.''