Ligi Tanzania,kuwa na msisimko

Image caption Emanuel Okwi mchezaji wa Simba anayetokea Uganda

Ligi kuu ya Tanzania Bara inategemewa kuwa na msisimko zaidi msimu ujao kwa mwaka 2015/16 baada ya bodi ya ligi nchini humo kupitisha azimio la kusajili wachezaji 10 wa kigeni.

Msimu uliopita wa ligi kuu, kila timu shiriki iliruhusiwa kusajili wachezaji wageni wasiozidi watano lakini azimio jipya, ambalo bado vilabu wamelikubali, litatoa fursa ya kusajili wachezaji 10 katika kile kinachoonekana kuleta ushindani.

Mkurugenzi wa mashindano wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema azimio hilo litawasilishwa katika kamati ya utendaji kwa ajili ya kupata ridhaa.

Hata hivyo, ongezeko hilo la wachezaji watano limeleta maoni tofauti kwa wadau wa soka, huku wengine wakisema kuwa mbali ya kuleta ushindani, pia litaua vipaji na kunyima fursa ya uchezaji kwa wachezaji wazawa.

Vilabu vikubwa nchini Tanzania kama vile Simba, Yanga na Azam zimekuwa zikisajili wachezaji wageni kwa ajili ya kuleta tija katika ushindani wao wa ndani na ule wa kimataifa.