Tuzo za ligi kuu Tanzania bara

Image caption Hans Pluijm akishangilia,je katika tuzo za ligi kuu Tanzania bara bado atafurahia?

Makocha wa kigeni, Hans Plujim kutoka Uholanzi anayeifundisha timu ya Yanga na Goran Kopunovic, aliyekuwa kocha wa Simba ambaye kwa sasa amerudi nyumbani kwao, wapo katika kinyang’anyiro cha kugombania tuzo ya kocha bora wa ligi kuu ya Tanzania Bara itakayotolewa Jumatano jioni wiki hii.

Mbali na makocha hao, pia yupo kocha mzawa, Mbwana Makata aliyekuwa Prisons kuwania tuzo ya kocha bora wa ligi hiyo iliyokwisha mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Afrisa Mawasiliani wa Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, TFF, kwa kushirikiana bodi ya ligi na wadhamini watatoa zawadi kwa timu, wachezaji na makocha waliofanya vizuri katika msimu ulioisha hivi karibuni.

Mshambuliaji mpya wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mrisho Khalfan Ngassa atawania tuzo ya Mchezaji Bora dhidi ya mfungaji bora wa Ligi hiyo, Simon Msuva.

Ngassa na Msuva wote walikuwemo kwenye kikosi cha Yanga SC kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliomalizika Mei mwaka huu na watachuna na beki chipukizi wa Simba SC, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’

Utoaji wa tuzo hizo utafanyika katika ukumbi wa JB Belmonte (Kilimanjaro) uliopo katika jengo la Golden Jubilee Tower (PSPF), mtaa wa Ohio, Dar es Salaam kuanzia saa 12:00 jioni.

Kipa chipukizi, Mohamed Yusuph wa Tanzania Prisons atachuana na Said Mohamed wa Mtibwa Sugar na Shaaban Kado wa Coastal Union kuwania tuzo ya kipa bora.

Israel Nkongo atachuana na Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu kuwania tuzo ya Refa Bora, wakati Mgambo JKT, Mtibwa Sugar na Simba SC zitagombea tuzo ya timu yenye Nidhamu.

Pamoja na tuzo binafsi, Vodacom ambao ni wadhamini wa Ligi Kuu tangu mwaka 2002, watatoa zawadi kwa Bingwa (Yanga) mshindi wa pili (Azam) , mshindi wa tatu Simba na na mshindi wa nne.