Kocha wa Taifa Stars afukuzwa

Image caption Kufuzu AFCON: Uganda yaifunga Tanzania, kocha Nooij, wasaidizi wake watimuliwa

Kipigo cha magoli 3-0 ilichokipata timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kutoka timu ya Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya CHAN kimesababisha kufukuzwa kwa kocha wa timu hiyo, Mdachi Mart Nooij.

Nooij alikuwa akikali kuti kavu katika benchi la ufundi la timu hiyo baada ya kufanya vibaya katika mechi kadhaa, zikiwemo zile za Michuano ya Cosafa ya Afrika ya Kusini, kufungwa 3-0 na Misri katika mechi za kufuzu kucheza fainzali za AFCON 2017 na Jumamosi kupokea kipigo kama hicho (3-0) kutoka kwa Uganda katika mechi iliyochezwa usiku Jumamosi visiwani Zanzibar.

Kufutia kipigo hicho, kamati ya utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao chake kilichofanyika Jumamosi usiku muda mfupi baada ya mechi, kujadili pamoja na mambo mengine, mwenendo wa Taifa Stars ikiwa ni pamoja na kuufanyia tathmini mchezo huo , Stars vs Uganda.

Kwa mujibu wa msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, kamati ya utendaji kwa kauli moja imeamua kusitisha ajira ya Kocha Mkuu Maart Nooij tarehe 21/June/2015.

Maamuzi mengine ni pamoja na kulivunja benchi lote ufundi la Taifa stars .

Kizuguto amesema uongozi wa TFF utatangaza punde benchi jipya la ufundi la timu ya Taifa.

Stars inakabiliwa na mechi ya marudiano na Uganda jijini Kampala baada ya wiki mbili na pia itacheza tena na Misri jijini Dar es Salaam baada ya miezi kadhaa ijayo