Arsenal kumlipa Wilshere £100,000

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wilshere

Arsenal itapuuzilia mbali hamu ya Manchester City ya kutaka kumsajili kiungo wake wa kati Jack Wilshere kwa kumpatia mkataba mwengine wa miaka mitano pamoja na kuongeza mshahara wake mara mbili ya anavyopata.

Kulingana na gazeti la the Mirror, Manchester City ambayo ilishindwa kutetea taji lake la ligi msimu uliopita ina hamu ya kuimarisha safu yake ya kati kwa kununua wacheza wa Uingereza katika uwanja wa Etihad na Wilshere ni miongoni mwa wachezaji inaowalenga pamoja na Raheem Sterling wa Liverpool na Fabian Delph wa Aston Villa.

Lakini the Gunners wako tayari kumzuia Wilshere mwenye umri wa miaka 23 ambaye amekuwa kiungo muhimu cha timu hiyo na taifa lake.

Baada ya kukaa nje kwa miaka miwili na jeraha,Wilshere ameonyesha kwamba yuko imara kwa mara nyengine tena baada ya kuifungia Uingereza mabao 2 dhidi ya Slovenia katika mechi ya kufuzu kwa michuano ya Ulaya.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Etihad

Iwapo Manchester City itashindwa kumpata Wilshere basi Sterling atakuwa windo lake.

Lakini Arsenal inajua hatari ya kumkosa mchezaji huyo na tayari imeanza mazungumzo ya kumpatia mkataba mpya.

Wilshere bado ana miaka mitatu ya mkataba wake katika uwanja wa Emirates lakini Arsenal iko tayari kuimarisha malipo yake na kufikia pauni 100,000 kwa wiki ili kuhakikisha kuwa anasalia .