Micho ajinasibu kwa yaliyopita

Image caption Kocha Micho akiwa na wachezaji wake

Kocha wa Uganda, Milutin 'Micho' Sredojevic amesema timu yake, The Cranes ilicheza kwa umakini na kuweza kuwafunga wenyeji wao Taifa Stars ya Tanzania 3-0 katika mchezo wao wa kwanza wa kogombania nafasi ya kufuzu kucheza fainali za michuano ya CHAN mwaka 2016 nchini Rwanda.

Micho amesema wachezaji wake walitumia vizuri nafasi walizopata dhidi ya Stars wakiwa nyumbani katika mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi usiku visiwani Zanzibar.

“Tulicheza kwa umakini kwa kuwa tulijua tupo ugenini na tulihitaji ushindi ili kujiweka vizuri na mechi yetu ya marudiano wiki mbili zijazo jijini Kampala”, amenukuliwa Micho akisema.

Mabao mawili ya mshambuliaji Erisa Sekisambu na lingine la Farouk Miya yaliiwezesha Uganda kushinda 3-0. Stars, ambayo imekatisha mkataba na kocha wake, Mholanzi Mart Nooij, inahitaji ushindi wa magoli 4-0 ili iweze kusonga mbele.