Mchezaji wa raga afariki Australia

Image caption Mchezaji wa raga aliyefariki baada ya kujeruhiwa katika mechi

Mchezaji wa raga wa ligi kuu nchini Australia, ambaye alipata majeraha mabaya katika mchuano wa kuwania kombe la Queensland nchini humo, amefariki hospitalini.

James Ackerman, mwenye umri wa miakia 25, alikuwa akiichezea timu ya Sunshine Coast Falcons, alipopata majeraha mabaya ya kichwa dakika tano tu baada ya kuanza kwa mechi dhidi ya timu ya Norths Devils.

Mchezaji huyo aliye na watoto wawili, alitibiwa katika uwanja wa Bishop Park, kabla ya kukimbizwa Hospitalini mjini Brisbane.

Mechi hiyo iliofanyika siku ya Jumamosi ilisitishwa.

Wakuu wa Queensland Rugby League (QRL) wametangaza rasmi leo Jumatatu kwamba, Ackerman ameaga dunia.

Kwa mjibu wa gazeti la Courier-Mail linalochapishwa mjini Australia , Francis Molo, mwenye umri wa miaka 20, na ambaye alikabiliana na Ackerman na kusababisha majeraha hayo, ameingiwa na wasiwasi mkubwa.

Mkurugenzi mkuu wa Sunshine Coast Falcons, Chris Flannery, amemuelezea Ackerman kama "bingwa" na "mmojawepo wa viongozi wetu".