Keshi na Enyeama wasubiri uamuzi wa NFF

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Keshi na Enyeama

Mkufunzi wa timu ya soka nchini Nigeria Stephen Keshi amekutana na kamati ya nidhamu ya shirikisho la kandanda nchini humo, NFF mapema leo jumanne, ili kujibu maswali kuhusiana na kuwepo kwa jina lake katika orodha ya wasimamizi wa soka nchini Ivory Coast.

Hata hivyo mlinda lango Vincent Enyeama amekataa kufika mbele ya jopo hilo ili kujibu maswali kuhusiana na matamshi aliyotoa ya kucheza mechi ya kimataifa mjini Kaduna.

Halmashauri kuu ya Shirikisho la NFF itakuwa na usemi wa mwisho wa adhabu ya aina yoyote katika tarehe ambayo haijatangazwa bado.

Keshi, ambaye ametia saini ya miaka miwili na NFF mwezi April mwaka huu, alikuwa katika orodha ya watu 59 walioomba kazi ya ukufunzi na iliyochapishwa majuzi na shirikisho la kandanda nchini Ivory FIF ili kuchukua mahala pa Raia wa Ufaransa Herve Renard.

Wakati huo huo, nahodha wa Super Eagles, Enyeama ametoa "matamshi ya kejeli" kuhusiana na usalama mjini Kaduna kwa mechi ya kufuzu kwa mchuano wa mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 dhidi ya Chad.

Enyeama, anayesakata dimba ya kulipwa na klabu ya Lille ya Ufaransa ni mchezaji bora zaidi wa Super Eagles, kwani ameichezea timu yake mara 101, hajajibu kabisa Shirikisho la NFF, linalomtaka kuelezea kwa kina matamshi yake hayo.