Taifa Queens itaruka kihunzi Namibia?

Image caption wachezaji wa netball wa Tanzania.

Chama cha netball Tanzania (Chaneta) kimesema kina imani timu ya taifa, Taifa Queens itapeperusha vema bendera ya nchi hiyo katika michuano ya Afrika itakayofanyika nchini Namibia June 28.

Timu hiyo inategemewa kukabidhiwa tiketi Jumatano tayari kwa safari ya kuelekea Windhoek, Namibia kati ya Alhamisi au IJumaa wiki hii, kwa mujibu wa kiongozi mkuu wa Chaneta, Anna Kibira.

Kiongozi wa chama cha mchezo huo Tanzania Bara (Chaneta), Anna Kibira amesema kuwa watachagua timu kwa kushirikiana na wenzao wa Zanzibar (Chaneza) kwa ajili ya kuanza kambi hapo Mei 17 visiwani Zanzibar.

Tanzania iliombwa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo kabla ya kuhamishiwa Namibia, lakini imeshindwa kutokana na uhaba wa fedha.Awali, Zambia iliteuliwa kuwa mweyeji kabla ya Tanzania kuombwa na ilishindwa kwa sababu kama hizo.

Tanzania ilishindwa kushiriki michuano hiyo ya mwaka 2013 iliyofanyila Blantyre, Malawi kutokana na ukosefu wa fedha , lakini Kibira amesema watafanya jitihada ili kuhakikisha wanasafiri kwenda Namibia kushiriki. Nchi mbalimbali za Afrika kama vile Kenya, Uganda zinategemewa kushiriki michuano hiyo.