Taifa Stars yaalikwa Ubalozini Uganda

Image caption Taifa Stars ya Tanzania

Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda umeikirimu timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) chakula cha jioni baada ya timu hiyo kutolewa na Uganda (The Cranes) katika kinyang'anyiro cha kugombania nafasi ya kucheza fainali cha CHAN mwakani nchini Rwnada.

Katika mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa katika uwanja wa Nakivubo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 na Tanzania kuanga michuano hiyo, baada ya kipigo cha magoli 3-0 ilichokipata kutoka kwa Uganda wiki mbili zilizopita mjini Zanzibar. Stars ilialikwa chakula cha jioni na ofisi ya Ubalozi wa Tanzania iliyopo jijini Kampala.

Katika hafla hiyo ya chakula cha jioni, wenyeji wakiwemo maofisa wa ubalozi , watanzania waishio nchini Uganda waliwapongeza wachezaji, viongozi kwa mchezo mzuri dhidi ya Uganda na kuwatakia kila la kheri katika safari ya jumatatu ya kurejea jijini Dar es salaam ikitokea Uganda kwa Shirika la ndege la Rwandair.