Tanzania yajitoa All Africa Games .

Image caption Waendesha baiskeli Tanzania wajitoa michezo ya Afrika

Chama cha mchezo wa baiskeli nchini Tanzania kimejitoa kushiriki michezo ya Afrika (All Africa Games) itakayofanyika mapema mwezi Septemba nchini Congo Brazzaville.

Katibu mkuu wa Kamati ya Olimpiki nchini Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema uongozi wa chama hicho umeitaarifu kamati yake juu ya kutoshiriki michuano hiyo itakayoanza September 4-19.

Ukosefu wa fedha umekuwa ni kikwakzo kwa vyama vingi vya michezo nchini Tanzania kushiriki katika michezo mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ya kufuzu michuano mbalimbali ikiwemo hiyo ya Afrika na mengineyo kama vile ya Olimpiki na Jumuiya ya Madola.

Serikali inategemewa kugharamia ushiriki wa wanamichezo kuelekea katika michezo hiyo lakini mpaka sasa haijajulikana ni wanamichezo wangapi watashirki.

Mbali ya baiskeli, Tanzania inategemewa kushiriki katika michezo ya taekwondo, kuogelea, riadha, ngumi na michezo ya watu wenye ulemavu.