Wanariadha wawili wa Kenya Matatani

Joyce Jakary Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mwanariadha wa Kenya aliyenaswa na WADA

Wanariadha wawili wa Kenya wamepigwa marufuku ya muda ya kutoshiriki katika shindano lolote la riadha, baada ya kupatikana na hatia ya kutumia madawa yaliyoharamishwa ya kusisimua misuli.

Shirikisho la mchezo wa riadha duniani IAAF, lisema wawili hao Joyce Zakary na Koki Manunga, wamekubali adhabu hiyo, baada ya kufahamishwa matokeo ya uchunguzi uliofanywa katika hoteli wanamoishi mjini Beijing.

Maafisa wa kupamabana na matumizi ya madawa hayo, michezoni waliwafanyia uchunguzi wanariadha hao walioshiriki katika mbio za mita mita nne na mita mia nne kuruka viunzi tarehe Ishirini na Ishirini na moja mwezi huu.

Zakary aliweka rekodi mpya ya kitaifa katika mbio hizo pale alipotumia muda wa sekunde 50.71 katika hatua ya mchujo ya mbio za mita mia nne, siku ya Jumatatu.

Hata hivyo mwanariadha huyo hakushiriki katika mbio za nusu fainali siku ya Jumanne.

Huwezi kusikiliza tena

Manunga naye alimaliza mbizo za mita mia nne kuruka viunza katika nafasi ya sita kwa kutumia muda wa sekunde 58.96.

Shirikisho la mchezo wa riadha nchini Kenya AK, tayari limefanya mashauriano na IAAF na wanariadha hao wawili.

AK tayari imeanzisha uchunguzi kubainisha hali iliyosababisha wanariadha hao kupatikana na hatia.

Kwa sasa wanariadha kumi na watatu wa Kenya wamepigwa marufuku ya kushiriki katika shindano lolote, kuhusiana na matumizi ya dawa hizo zilizoharamishwa.

Shirika la kudhibiti matumizi ya dawa hizo michezoni WADA limetangaza kuwa litaanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya kusambaa kwa uhalifu huo michezoni.