Timu ya raga yakumbwa na kashfa ya ubaguzi-AK

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Timu ya raga ya Afrika Kusini

Chama kimoja cha kisiasa nchini Afrika Kusini, kimewasilisha kesi mahakamani, kuzuia timu ya taifa ya mchezo wa raga, kutoshiriki katika fainali za kombe la dunia itakayoandaliwa mjini London.

Chama cha New Agenda, ambacho kinajumuisha wanachama waasi wa chama tawala cha ANC, kimewasilisha kesi mahakama, kutaka wachezaji na maafisa wa timu hiyo kuwasilisha pasi zao za usafiri na pia kuzuiwa kusafiri Uingereza kwa fainali hizo za dunia.

Kesi hiyo sasa itasikilisha siku ya Jumatano.

Chama hicho ambacho kimekataa kutoa idadi ya wanachama wake, kimemshtaki maafisa wakuu wa shirikisho la mchezo huo nchini Afrika Kusini na waziri wa michezo.

Chama hicho kimenadi kuwa uteuzi wa wachezaji katika kikosi hicho ulikumbwa na ubaguzi wa rangi.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kocha wa Afrika Kusini, Heyneke Meyer

Kocha wa timu hiyo Heyneke Meyer, alitaja kikosi chake, kinachojumuisha asilimia 30 ya wachezaji ambao sio wazungu, kuambatana na sheria za nchi hiyo.

Lakini chama hicho kinataka mahakama kuagiza kubuniwa kwa tume kuchunguza suala hilo.

Kandanda ni mchezo ambao unapendwa na raia wengi weusi huku mchezo wa raga nao ukivutia idadi kubwa ya wazungu, lakini kumekuwa na juhudi za kuvunja dhana hii ya ubaguzi.

Msemaji wa wizara ya michezo amesema ni muhimu kwa raia wote wa nchi hiyo kuunga mkono timu zao za taifa,bila kuzingatia rangi au kabila wito ambao pia ulitolewa na aliyekuwa rais wa kwanza mweusi, Hayati Nelson Mandela mwaka wa 1995 wakati wa fainali za kombe la dunia.

Licha ya chama hicho kudai kuwa ina sababu za kutosha kuwasilisha kesi hiyo, wakosoaji wanasema kuwa chama hicho cha New Agenda, kinajaribu kujinufaisha kwa kupewa nafasi nya vyombo vya habari, na hivyo kuhujumu juhudi za kutokomeza ubaguzi wa rangi michezoni nchini humo.