Man Utd 'hawaelewi kuhama kwa wachezaji'

David De Gea
Image caption David De Gea hakufanikiwa kuhamia Real Madrid

Rais wa kilabu ya Real Madrid amesema Manchester United hawana uzoefu kuhusu kuhama kwa wachezaji na ndiyo sababu uhamisho wa David De Gea ulitibuka.

Florentino Perez aligusia pia kushindwa kwa United kusajili Fabio Coentrao kutoka Real na Ander Herrera wa Athletic Bilbao siku ya mwisho ya kuhama wachezaji mwaka 2013.

Uhamisho wa De Gea ulitibuka kwa kuwa stakabadhi zake hazikuwasilishwa kwa wakati.

"Hawana uzoefu," Perez aliambia redio ya Uhispania ya Cadena SER.

"Jambo sawa lilitendeka kwa Coentrao na Herrera."

Real na United wamekuwa wakiwekeana lawama kwa kuchelewa kwa stakabadhi za kukamilisha uhamisho wa De Gea.

Kilabu hiyo ya Uhispania inasema ilifanya kila ililoweza kumsajili mlinda lango huyo wa miaka 24 kwa £29, lakini ikachelewa kwa dakika mbili.

United, waliotaka kumsajili Keylor Navas kama sehemu ya mkataba huo, nao walisema waliwasilisha stakabadhi zote dakika mbili kabla ya muda wa mwisho kupita.

Perez alisema Red Devils walikubali tu kumuuza kipa huyo saa 12 kabla ya soko la kuhama wachezaji kufungwa Uhispania, na kisha wakachukua saa nane kurejesha stakabadhi.

Haki miliki ya picha epa
Image caption Ander Herrera alishindwa kuhamia Utd 2013

Rais huyo wa Real pia alidai United walikuwa wameonyesha ishara za kutaka kusajili mshambuliaji wa Wales Gareth Bale pamoja na Wafaransa Karim Benzema na Raphael Varane kutoka kwao.

Makamu mwenyekiti mtendaji wa United Ed Woodward alishindwa kuwasajili Herrera na Coentrao majira ya joto ya 2013, wakati wake wa kwanza kuwa sokoni baada ya kuchukua pahala pa David Gill.

Iliripotiwa kwamba uhamisho wa Herrera ulivurugika baada ya matapeli, waliojidai kuwakilisha United, kufika afisi za wasimamizi wa ligi ya Uhispania. United waliambulia patupu kumchukua Coentrao baada yao kushindwa kukamilisha uhamisho wake kwa wakati.

Kiungo wa kati huyo Herrera, 26, hatimaye alihamia kilabu hiyo ya Ligi ya Premia Juni 2014.

United wamesema watabadilisha sera yao ya uendeshaji shughuli sokoni na kuangazia zaidi wachezaji nyota siku za usoni.