Mario Gemina kuchezea Gabon

Haki miliki ya picha
Image caption Mario Lemina

Mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20, Mario Lemina, ametangaza kuwa amebadili uamuzi wake wa kutoichezea timu ya taifa ya soka ya Gabon.

Januari mwaka huu, Lemina alikataa kujiunga na kikosi cha Gabon kilichoshirika katika kombe la mataifa ya Afrika, kwa matarajio kuwa huenda angelijumuishwa kwenye kikosi cha Ufaransa.

Lakini mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 22, aliyejiunga na Juventus kwa mkopo tarehe 31 mwezi uliopita, sasa ametangaza kuwa ataichezea timu hiyo ya taifa ya Gabon.

Amesema tayari amesaini mkataba na shirikisho la mchezo wa soka la Gabon na kwa sasa anasubiri mechi yake ya kwanza na timu hiyo.

Chini ya sheria za shirikisho la mchezo wa soka duniani FIFA, Lemina anaweza kuichezea taifa lolote kwa sababu hajawahi kuichezea timu ya taifa ya taifa lolote.

Gabon ni mwenyeji wa fainali za kombe la Mataifa ya Afroka mwaka wa 2017, miaka mitano tu baada ya kuandaa fainali hizo kwa pamoja na Equitorial Guinea.

Lemina alianza kucheza kwenye ligi za kulipwa na klabu ya Lorient na aliichezea timu hiyo kwa muda wa miaka minane.

Aliondoka Lorient na kujiunga na Marseille Agosti mwaka wa 2013 na kufunga mabao mawili baada ya kucheza mechi 50 na klabu hiyo kabla ya kujiunga na Juventus kwa mkopo.