Mourinho: Nilisahau utamu wa ushindi

Jose Mourinho Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Chelsea wameshinda mechi moja pekee ligi ya Uingereza

Mkufunzi mkuu wa Chelsea Jose Mourinho amesema alikuwa amesahau utamu wa ushindi akizungumza baada ya vijana wake kujikwamua na kupata ushindi wa 4-0 dhidi ya Maccabi Tel Aviv.

Hii ni baada ya kilabu hiyo kuanza vibaya ligi ya Premier ikishinda mechi moja pekee kati ya tano ilizocheza.

"Nilikuwa nimesahau mtu anavyohisi. Kwa muda mrefu hatukushinda mechi, inahisi vyema sana, ni hisia nzuri,” alisema Mourinho.

“Mimi huwa meneja mzuri ninaposhinda mechi na husalia meneja mzuri ninaposhindwa.”

Licha ya kuanza kwa mkosi wa Eden Hazard kupoteza penalti, mabao ya Willian, Oscar, Diego Costa na Cesc Fabregas yaliwawezesha Chelsea kuwalemea wapinzani hao kutoka Israel mechi yao ya kwanza Ligi ya Kilabu Bingwa Ulaya msimu huu.

"Penalti tuliyopoteza ilikuwa mtihani mkubwa sana kwetu,” Mourinho akaongeza. “Unapoanza mechi ambayo unahitajika sana kushinda na baada ya dakika tano unapoteza mechi, ni kisa cha kuvunja moyo lakini tulijibu vyema.”

Mourinho alikuwa ameangaziwa sana kabla ya mechi hiyo baada ya kilabu yake kuanza ligi vibaya zaidi tangu 1986.

Licha ya hayo, mashabiki waliohudhuria mechi hiyo ya Ulaya uwanjani Stamford Bridge bado waliimba na kumsfu jina lake lilipotajwa kabla ya mechi kuanza na walimuunga mkono mechi yote.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Oscar ni mmoja wa waliofungia Chelsea

Akiongea baadaye, Mourinho alisema anafurahia mashabiki wanapomuunga mkono badala ya wanapoimba ‘Mourinho aende’ na kumzomea.

“Hili linaonyesha hawasomi magazeti au hawasahau haraka. Iwapo hawasomi magazeti, wananiunga mkono. Iwapo hawasahau upesi, wananiunga mkono,” akasema.

"Tulishinda mataji manne la Ligi ya Premier, matatu tukiwa naye na moja na timu yake. Huyu si jamaa mbaya. Tuunge mkono jamaa huyu. Tuna nafasi ya kushinda taji la tano,” akaongeza Mourinho, akiashiria yaliyo akilini mwa mashabiki wanaoendelea kumuunga mkono.

Chelsea ilikuwa ndiyo kilabu ya pekee kutoka Uingereza kushinda mechi za kwanza Ligi ya Kilabu Bingwa Ulaya baada ya Arsenal kulazwa 2-1 na Dinamo Zagreb na kujiunga na Manchester United na Manchester City katika kujikwaa.

Mourinho hata hivyo alisema angelipendelea kilabu hizo zishindwe mechi za ligi ya Premier badala ya Ligi ya Kilabu Bingwa Ulaya.