Kocha apigwa marufuku na Caf kwa kutusi refa

Logo ya Caf
Image caption Kwenye kikao cha majuzi Caf ilitoza watu faini za jumla ya US$195,000

Kocha wa Guinea-Bissau Paulo Torres amepigwa marufuku kwa mechi zilizosalia zaza Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2017 kwa kumtusi refa.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lilimpata Torres na hatia ya “kutumia lugha ya kuudhi na matusi dhidi ya refa.”

Kisa hicho kilitokea wakati wa mechi dhidi ya Zambia ambayo iliisha sare tasa.

Torres atakosa mechi ya nyumbani na ya ugenini dhidi ya Kenya mwezi Machi mwaka ujao na kisha mechi dhidi ya Congo na Zambia.

Sare hiyo ya Guinea-Bissau iliwaacha wakishika mkua Kundi E na alama moja. Ni mshindi wa kundi pekee ambaye amehakikishiwa nafasi ya kushiriki fainali hizo za 2017 nchini Gabon.

Hata hivyo marufuku hiyo ya Caf haiathiri mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 na Torres yuko huru kuongoza timu hiyo dhidi ya Liberia kwenye raundi ya kwanza.

Guinea-Bissau watasafiri Liberia mnamo Oktoba 8 na kucheza mechi ya marudiano siku tano baadaye.