Chelsea yamtetea Mourinho licha ya masaibu

Jose Mourinho Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mourinho anakabiliwa na shinikizo baada ya Chelsea kushindwa kutamba msimu huu

Chelsea imesema inamuunga mkono meneja Jose Mourinho baada ya klabu hiyo kukumbana na mwanzo mbaya zaidi wa ligi tangu 1978-79.

Klabu hiyo ilijipata nambari 16 ligini ikiwa na alama nane baada ya kulazwa 3-1 na Southampton Jumamosi.

Baada ya kichapo hicho, Mourinho aliambia Sky Sports kuwa klabu hiyo italazimika kumfuta kazi iwapo inataka aondoke.

"Klabu hii ingependa kuweka wazi kwamba Jose anaendelea kuungwa mkono kikamilifu,” klabu hiyo ilisema kupitia taarifa fupi.

"Tunaamini tuna meneja afaaye na awezaye kubadili hali na kwamba ana wachezaji wa kufanya hilo.”

Baada ya mabingwa hao wa Ligi ya Premia kushindwa Jumamosi, Mourinho alisema: "Ninataka kusema wazi. Mwanzo, kwamba mimi si mtu wa kukimbia.

“Pili, iwapo klabu inataka kunifuta lazima inifute lakini mimi sitoroki majukumu yangu au timu yangu.”

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chelsea walichapwa 3-1 na Southampton Jumamosi

Hayo yakijiri, nahodha wa klabu hiyo John Terry pia amesema Mreno huyo wa umri wa miaka 52 ndiye afaaye Zaidi kusaidia klabu hiyo kujikwamua.