Liverpool wawasiliana na Jurgen Klopp

Jurgen Klopp
Image caption Ripoti zinasema Klopp yuko tayari kuanza kunoa klabu

Klabu ya Liverpool imewasiliana na wawakilishi wa Jurgen Klopp ikimtaka achukue nafasi ya meneja aliyefutwa kazi Brendan Rodgers.

Meneja huyo wa zamani wa Borussia Dortmund anapigiwa upatu kujaza nafasi iliyoachwa na raia huyo wa Ireland kaskazini, meneja wa zamani wa Chelsea Carlo Ancelotti akimfuata.

Klopp, 48, ambaye ni raia wa Ujerumani, anadaiwa kuwa tayari kuanza tena kazi.

Wamiliki wa klabu hiyo ya Anfield wanataka kuwa na meneja mpya wa kuandaa timu hiyo kwa mechi yao ya Ligi ya Premia ugenini Tottenham Oktoba 12.

Duru za karibu na Rodgers, 42, zinasema amesikitishwa sana na uamuzi wa kumfuta na anapanga kwenda kupumzika kwa muda kabla ya kuchukua kazi nyingine.

Alifutwa baada ya kuhudumu kama meneja kwa miaka mitatu unusu, baada ya timu yake kutoka sare ya 1-1 na Everton.

Mashauriano sasa yanatarajiwa kufanyika kati ya Rodgers na klabu hiyo kuhusu pesa atakazolipwa, ambazo huenda zikazidi £5m.

Wamiliki wa Liverpool kutoka Marekani Fenway Sports Group hawana mipango yoyote ya kusafiri Uingereza, na kwa sasa wanapanga kufuatilia shughuli ya kusaka meneja mpya kutoka Marekani.

Klopp anaripotiwa kuwasiliana na kiungo wa kati wa zamani wa Liverpool na Mjerumani mwenzake Dietmar Hamann kuhusu klabu hiyo, jiji na mashabiki.

Amekuwa hana kazi tangu kuondoka Dortmund majira ya joto, ambao alishinda mataji mawili ya Bundesliga akiwa nao.