Shangwe Arsenal baada ya kuchapa Bayern

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Arsenal walikuwa wameshindwa mechi zao za kwanza Uefa msimu huu

Arsenal walifufua matumaini yao katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa ushindi wa kusisimua dhidi ya Bayern Munich katika uwanja wa Emirates mechi iliyochezwa Jumanne usiku.

Matumaini ya Gunners yalikuwa yamefifia baada yao kushindwa mechi zao za kwanza katika ligi hiyo msimu huu ugenini Dinamo Zagreb na nyumbani dhidi ya Olympiakos.

Lakini vijana hao wa Arsene Wenger walionyesha bado hawako tayari kusalimu amri kwa kulaza Bayern, ambao wamekuwa wakiogopwa sana siku za karibuni.

Bayern walidhibiti mpira zaidi lakini Arsenal walifunga kupitia nuguvu mpya Olivier Giroud dakika ya 77 baada ya kipa Manuel Neuer kufanya kosa nadra sana na kushindwa kufikia frikiki iliyopigwa na Santi Cazorla.

Walijihakikishia ushindi sekunde za lala salama Mesut Ozil alipofunga kutokana na krosi ya Hector Bellerin.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Cech aliokoa mipira mingi hatari

Arsenal wanafaa kumshukuru sana kipa wao Petr Cech, aliyerejea kulinda michuma baada ya makosa ya David Ospina mechi yao dhdi ya Olympiakos, aliyeokoa mipira hatari kutoka kwa Thiago Alcantara na Arturo Vidal.

Neuer pia alikuwa amefanya miujiza yake kabla ya kosa hilo, akiokoa mpira wa kichwa wa Theo Walcott kwa ustadi mkubwa kipindi cha kwanza.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Huwa nadra sana kwa kipa Neuer kufanya makosa

Katika mechi nyingine, Chelsea walitoka sare tasa na Dynamo Kiev.

Haya ndiyo matokeo ya mechi zote za Ligi ya Klabu Bingwa zilizochezwa Jumanne:

BATE Bor 0 - 2 Barcelona

Bayer Levkn 4 - 4 Roma

Arsenal 2 - 0 Bayern Munich

Dynamo Kiev 0 - 0 Chelsea

Dinamo Zagreb 0 - 1 Olympiakos

FC Porto 2 - 0 Maccabi Tel Aviv

Valencia 2 - 1 KAA Gent

Zenit St P 3 - 1 Lyon