Liverpool waambulia sare Europa League

Liverpool Rubin Kazan Europa League Haki miliki ya picha Getty
Image caption Klopp amesema hakufurahishwa na matokeo hayo

Meneja mpya wa Liverpool Jurgen Klopp alishindwa kuandikisha ushindi mechi yake ya kwanza Anfield baada ya vijana wake kulazimishiwa sare ya 1-1 na Rubin Kazan katika Europa League.

Wageni wao walichukua uongozi kupitia Marko Devic lakini nahodha wao Oleg Kuzmin alifukuzwa uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano muda mfupi baadaye.

Liverpool walijibu kupitia Emre Can baada ya kuchapwa kwa frikiki.

Nguvu mpya Christian Beneteke alikosea pembamba kuwafungia la pili baada ya kombora lake kugonga mlingoti wa goli na mwishowe Liverpool wakakubali kuondoka na sare ambayo ndiyo ya tatu mtawalia katika mechi zao Kundi B.

Licha ya kujikakamua sana dakika za mwisho, haukuwa usiku mwema kwa Klopp na Liverpool kwani walishindwa kupenya ngome ya wapinzani wao vipindi virefu vya mechi hiyo.

Matokeo hayo yamewaacha Liverpool nambari mbili katika kundi lao wakiwa na alama tatu, alama nne nyuma ya viongozi FC Sion.

Liverpool sasa wametoka sare mechi saba kati ya nane walizocheza karibuni zaidi.

Akizungumza baadaye, Klopp alisema: "Unapoingia kwenye nyumba mpya, huwa unapokea zawadi. Sijafurahishwa na zawadi niliyoipata leo".

Kwenye mechi nyingine zilizochezwa Alhamisi, matokeo yalikuwa kama ifuatavyo:

Molde 3 - 1 Celtic

Anderlecht 2 - 1 Tottenham Hotspur

Liverpool 1 - 1 Rubin Kazan

Fenerbah├že 1 - 0 Ajax

Monaco 1 - 0 FK Qarabag

Apoel Nic 2 - 1 Asteras Tripolis

Schalke 2 - 2 Sparta Prague

AZ Alkmaar 0 - 1 FC Augsburg

Partizan Belgrade 0 - 2 Athletic Bilbao

Bordeaux 0 - 1 FC Sion

FK Qabala 1 - 3 Borussia Dortmd