Mourinho agomea wanahabari baada ya kushindwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Carroll alifunga bao lake kwa kichwa

Meneja wa Chelsea Jose Mourinho alikataa kuzungumza na wanahabari baada ya timu yake kushindwa 2-1 ugenini West Ham.

Vijana wake walimaliza wakiwa kumi uwanjani baada ya kiungo wa kati Nemanja Matic kuonyeshwa kadi mbili za njano.

Mourinho naye alifukuzwa eneo wanamokaa makocha uwanjani wakati wa kuanza kwa kipindi cha pili baada yake kujaribu kuzungumza na refa Jon Moss wakati wa mapumziko.

Mauro Zarate aliweka West Ham mbele dakika ya 17 baada ya Chelsea kushindwa kujilinda vyema wakati wa kupigwa kwa kona.

Gary Cahill alisawazisha dakika ya 56 lakini Carroll aliyeingia kama nguvu mpya alifikia krosi ya Aaron Cresswell na kufunga kwa kichwa dakika ya 79.

West Ham sasa wanashikilia nambari mbili kwenye jedwali kabla ya debi ya kesho kati ya Manchester City na Manchester United uwanjani Old Trafford.

Wachezaji wengine watano wa Chelsea pia walionyeshwa kadi za njano kwenye debi hiyo ya London magharibi, ya mwisho kuchezewa Upton Park kabla ya West Ham kuhamia Olympic Stadium majira yajayo ya joto.