Liverpool,Man City zashinda Man United nje

Image caption Kocha mpya wa Liverpool ya Uingereza,Jurgen Klopp, ameandikisha ushindi wake wa kwanza kama mkufunzi wa timu hiyo.

Kocha mpya wa Liverpool ya Uingereza,Jurgen Klopp, ameandikisha ushindi wake wa kwanza kama mkufunzi wa timu hiyo.

Kocha huyo aliyetokea Ujerumani alishangilia The Reds walipoibana Bournemouth bao 1-0 katika raundi ya nne ya mchuano wa kuwania kombe la Capital One.

Jurgen Klopp ambaye alikuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na kujeruhiwa kwa washambulizi wake Christian Benteke na Daniel Sturridge alipata ushindi wake wa kwanza kupitia kwa mkwaju wa mchezaji mpya Nathaniel Clyne.

Image caption Nathaniel Clyne alifungia Liverpool bao lake la kwanza

Klopp alikuwa na imani kuwa Roberto Firmino na mzaliwa wa Kenya Divock Origi wangempa matokeo mema.

Hata hivyo, Firmino na Origi walikosa makali mbele ya lango na Clyne akampa kocha huyo sababu ya kutabasamu.

The Reds, ambao wanashikilia rekodi ya klabu iliyoshinda kombe hilo la Capital One mara nyingi zaidi sasa wamefuzu kwa robo fainali ya mchuano huo kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Hapo jana Arsenal na Chelsea zilishindwa na hivyo kuondolewa katika mkumbo ujao wa mashindano hayo.

Image caption Middlesbrough ilifuzu kwa robo fainali ya kombe la Capital One baada ya kuwatamausha Manchester United mabao 3-1 kwa mikwaju ya penalti.

Kinyume cha furaha hiyo huko Anfield, kilio kilitanda Old Trafford Middlesbrough ilifuzu kwa robo fainali ya kombe la Capital One baada ya kuwatamausha Manchester United mabao 3-1 kwa mikwaju ya penalti. Mechi hiyo ilikuwa imeisha sare tasa. katika muda wa kawaida na ule wa ziada.

Wayne Rooney, Michael Carrick na Ashley Young wote walikosa penalti zao.

Image caption Wayne Rooney, Michael Carrick na Ashley Young wote walikosa penalti zao.

Middlesbrough ambayo ilishiriki ligi kuu ya Uingereza mara ya mwisho katika msimu wa 2008-09 haikuonesha udhaifu wowote kama ilivyokuw imetarajiwa.

Kimsingi licha ya kushindwa kwa wastani wa umiliki wa mechi hiyo 56% - 44 % na Mashetani wekundu , Vijana wa Aitor Karanka' walikuwa na nia ya kuthibitisha kuwa wangali na keke za kusakata dimba.

Waliwashambulia United kama nyuki.

Kwa jicho la mtazamaji, walihitaji mshambulizi mmoja tu mwenye hadhi ya ligi kuu na wangaibana United bila ya kuwa na sababu ya kusubiri hadi baada ya saa mbili uwanjani.

Hayo yote ni Kenda,

Image caption Middlesbrough ambayo ilishiriki ligi kuu ya Uingereza mara ya mwisho katika msimu wa 2008-09 haikuonesha udhaifu wowote

Middlesbrough waliokuwa wamekwenda Old Trafford wakiandamana na mashabiki takriban 10,000 ndio waliofuzu kwa mkondo ujao wa robo fainali.

Bila shaka itakuwa kwa furaha na hadhi fulani kwa mashabiki wa mahasimu wao wa jadi na majirani Manchester City kushiriki mkondo ujao huku wenzao wakiwa nje.

Hii ni kwa sababu Man City iliwavaa Crystal Palace kwa mabao 5-1 katika mechi iliyothibitisha kuwa wao ni videdea.

Kevin De Bruyne alifunga bao lake la 6 katika mechi 9 alizoshiriki za Manchester City.

Image caption Kevin De Bruyne alifunga bao lake la 6 katika mechi 9 alizoshiriki za Manchester City

Wilfried Bony ndiye aliyefungua mvua hiyo ya mabao kwa bao la kwanza alilofunga kwa kichwa mapema katika kipindi cha kwanza.

De Bruyne alifunga la pili kunako dakika ya 44 kabla ya kumsaidia Kelechi Iheanacho, kuihakikishia City nafasi katika mkondo ujao wa Capital One.

Mzee wa kazi na kigogo wa safu ya kati Yaya Toure, alifanya mambo kuwa 4-0 kupitia kwa mkwaju wa penalti naye Manuel Garcia akahitimisha kivuno hicho.

Image caption Southampton iliandikisha ushindi muhimu wa mabao 2 - 1 dhidi ya Aston Villa.

Licha ya bao la Damien Delaney Crystal Palace walikuwa butu mbele ya lango wakionesha mchezo hafifu.

Kocha Manuel Pellegrini sasa amenoa makali yake huku akijiandaa kuchuana na Norwich katika mechi ya ligi kuu.

Kwa upande wake Crystal Palace watakuwa na kila sababu ya kutahamaki watakapowaalika vijana wa Louis van Gaal wikiendi ijayo.

Katika mechi nyengine iliyochezwa leo Southampton iliandikisha ushindi muhimu wa mabao 2 - 1 dhidi ya Aston Villa.