Mourinho asema hana wasiwasi kuhusu kazi yake

Jose Mourinho Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mourinho amesema haelewi ni kwa nini wanahabari huchochea mameneja wafutwe

Meneja wa Chelsea Jose Mourinho amesisitiza kwamba hana wasiwasi kuhusu kazi yake kama meneja wa Chelsea huku klabu yake inapojaribu kufufua kampeni yao msimu huu.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Premia wanashikilia nambari 15 ligini na wameshina mechi tatu pekee ligini msimu huu.

“Sina wasiwasi kuhusu kazi yangu. Sina wasiwasi kuhusu mustakabali wangu,” Mourinho alisema huku klabu hiyo ikijiandaa kukabiliana na Liverpool Jumamosi.

"Huwa situmii hata sekunde moja katika siku yangu kufikiria kuhusu hilo.”

Ripoti zimedokeza kwamba meneja huyo wa umri wa miaka 52 huenda akafutwa kazi Chelsea wakishindwa na Liverpool.

Lakini Mourinho amekataa kusema iwapo amepewa hakikisho kutoka kwa bodi ya Chelsea na mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich kuhusu mustakabali wake.

Alipoulizwa na wanahabari kuhusu iwapo amepewa hakikisho kwamba hatafutwa, Mourinho alijibu: “Si lazima niwaambie.”

Mwezi Agosti, Mourinho alitia saini mkataba mpya wa miaka mine wa kumuweka Stamford Bridge hadi Juni 2019, lakini klabu yake imeanza vibaya sana kampeni ya kutetea taji la ligi.

Abramovich anajulikana kwa kuwafuta mameneja wanaoshindwa kuhakikisha Chelsea inamaliza katika nne bora.