Aston Villa wamchukua kocha wa zamani wa Lyon

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Sherwood alifutwa baada ya kusimamia Villa kwa miezi tisa pekee

Aston Villa watamteua mkufunzi wa zamani wa Lyon Remi Garde kuwa kocha wao mpya leo, kujaza nafasi ya Tim Sherwood aliyefutwa kazi.

Mfaransa huyo atatia saini mkataba wa miaka mitatu unusu na atafuatilia mechi ya Jumatatu dhidi ya Tottenham ugenini kutoka eneo wanamoketi mashabiki.

Mkufunzi huyo wa miaka 49 anachukua klabu hiyo ikiwa inashika mkia Ligi ya Premia baada ya kushinda alama nne pekee kutoka kwa mechi 10.

Kocha wa Bastia Reginald Ray ndiye atakayekuwa msaidizi wa Garde na wawili hao watasimamia mechi yao ya kwanza nyumbani dhidi ya Manchester City Jumapili ijayo.

Garde alisaidia Lyon kumaliza nambari nne, tatu na tano katika misimu mitatu aliyokuwa nao kuanzia 2011 kabla ya kuwaacha 2014 kutokana na sababu za “kibinafsi na kifamilia”.