Rosberg amshinda Hamilton nchini Mexico

Nico Rosberg Haki miliki ya picha AP
Image caption Ushindi huo ni kitulizo kwa Rosberg ambaye ni mara ya kwanza kushinda katika mbio tisa za karibuni zaidi

Nico Rosberg alipata ushindi wake wa kwanza kabisa katika muda wa miezi minne baada ya kumshinda mwenzake wa Mercedes Lewis Hamilton katika mashindano ya magari yaendayo kasi ya Mexican Grand Prix.

Mjerumani huyo alidhibiti mbio hizo kuanzia mwanzo, bingwa mpya wa dunia Hamilton akimfuata unyounyo lakini hakuweza kumpita.

Ushindi huo wa Rosberg, ambao ndio wake wa nne msimu huu, umemrejesha katika nambari mbili kwenye kinyang’anyiro cha kusaka ubingwa akiwa nyuma ya Sebastian Vettel wa Ferrari ambaye hakuweza kumaliza mbio hizo.

Valtteri Bottas wa Williams anashikilia nafasi ya tatu.

Tukio la kusisimua kwenye mbio hizo lilikuwa ni uhasama uliotarajiwa kwenye kambi ya Mercedes kati ya Rosberg na Hamilton.

Timu hiyo ilikuwa imeamua kutua mara moja pekee lakini wakiwa wamesalia na mizunguko 25 kati ya mizunguko 71 waliyokuwa wakikimbia, Mercedes walimtaka Rosberg kusimama mara ya pili.

Mzunguko uliofauata walimtaka Hamilton pia asimame.

Hamilton alipinga ombi la hilo lakini mwishowe hakuwa na budi kwani aliambiwa lilikuwa “agizo” kwa sababu za kiusalama.

Ushindi huo ndio wa kwanza kwa Rosberg tangu mbio za Austrian Grand Prix, mbio tisa zilizopita, na ushindi wake wa nne msimu huu.

Hamilton ameshinda mbio 10 kipindi hicho, na Rosberg bila shaka atafurahi sana kwani ni kitulizo baada ya kushuhudia Hamilton akishinda taji zikiwa zimesalia mbio tatu nchini Marekani wiki moja iliyopita, ushindi huo akiupata kutokana na kosa la Mjerumani huyo.

Hiyo ilikuwa Grand Prix ya kwanza kuandaliwa Mexico katika kipindi cha miaka 20.