Man United: van Gaal ''mimi si kiziwi''

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mkufunzi wa Manchester United Louis van Gaal amefichua kuwa anatambua mashabiki wa klabu hiyo hawajafurahia mbinu zake.

Mkufunzi wa Manchester United Louis van Gaal amefichua kuwa anatambua mashabiki wa klabu hiyo hawajafurahia mbinu zake.

va Gaal aliongezea kusema kuwa ushindi wao dhidi ya CSKA Moscow ulileta tabasamu Old Trafford.

Uamuzi wa kocha huyo kumuondoa Anthoy Martial na badala yake kumleta Fellaini mechi ikiwa 0-0 ulishtumiwa vikali huku mashabiki wakionyesha hisia zao kwa kumzomea.

Rooney aliipa United goli la kipekee na la ushindi kunako dakika ya 79.

"Mimi si kiziwi. Naelewa maoni ya mashabiki lakini mwishowe watafurahia," alijitetea Van Gaal.

Bao la Rooney ambalo lilikuwa goli lake la 237 katika timu hiyo na kumweka katika nafasi ya pili pamoja na Denis Law kwenye orodha ya wafungaji bora wa United, lilikuwa la kwanza la klabu hiyo baada ya muda wa dakika 404.

Man United iliandikisha matokeo ya kutofungana kwenye mechi zake dhidi ya Manchester City, Middlesbrough na Crystal Palace.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Rooney aliipa United goli la kipekee na la ushindi kunako dakika ya 79.

Bao la mwisho kabla ya ukame wa magoli lilifungwa na Anthony Martial mnamo tarehe 21 Oktoba wakichea dhidi ya CSKA Moscow

Mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Paul Scholes amelaumu mbinu za Van Gaal kwa kusababisha ukosefu wa ubunifu katika timu hiyo.

Uamuzi wake wa kumchezesha Martial katika wingi ya kushoto na kumtumia Rooney kama mshambuliaji pekee umevutia shinikizo kutoka wafuasi wa klabu hiyo.

Kiungo wa timu ya taifa ya Ufaransa, Anthony Martial amecheza pamoja na Rooney kwenye safu ya ushambulizi lakini kuondolewa kwake katika dakika ya 66 iliwakashirisha mashabiki ambao waliimba jina lake wakiwataka wachezaji wa klabu hiyo kushambulia Zaidi.

"Niko na furaha kwa sababu nimechezesha Rooney kushambulia na amefunga,’’ aliongeza Van Gaal.