Atiati katika timu ya baiskeli ya Rwanda

Image caption Timu ya mbio za baiskeli ya Rwanda kugoma

Waendeshaji baiskeli wa timu ya taifa ya Rwanda watishia kususia mashindano ya kimataifa ya 'tour of Rwanda', wiki moja kabla ya mashindano hayo kuanza kutimua vumbi.

Waendeshaji baiskeli 13 kati ya 15 wametangaza kususia mashindano ya hayo hadi pale watakapopewa dola 3000 za marekani kama kiinuamgongo.

Tayari Waendeshaji baiskeli hao wametoka katika kambi ya mazoezi ya timu ya taifa.

Chama cha mbio za baiskeli nchini Rwanda kimetangaza kusikitishwa na uamuzi huo.

Hata hivyo kimesema bora kuanza upya kutengeneza kikosi kingine kuliko kwendelea kuwategemea Waendeshaji baiskeli wasio na moyo na ari ya kupigania taifa.

Miongoni mwa Waendeshaji baiskeli hao ni Hadi Janvier nahodha wa timu ya taifa,Valens Ndayisenga bingwa mtetezi wa mbio hizo na bingwa mara nne wa 'Tour of Rwanda' Abraham Ruhumuriza.

Wanabaiskeli nchini Rwanda wanasifiwa sana kwa kupandisha hadhi ya taifa hilo kimchezo kuliko michezo mingine.

Lakini wamekuwa wakilalamikia pesa wanazopewa katika timu ya taifa ambazo hazilingani hata kidogo na zile zinazopewa wachezaji wa soka.

Mashindano ya mbio za baiskeli ya 'Tour of Rwanda' ni miongoni mwa mashindano maarufu sana,siyo tu nchini Rwanda bali pia barani afrika ambapo alama zake huhesabiwa katika kushindania ubingwa wa bara zima.