Blatter alazwa kwa kupata mshituko

Haki miliki ya picha r
Image caption Sepp Blatter

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Sepp Blatter amelazwa hospitalini kutokana na kupatwa mshituko wa neva.

Blatter aliyesimamishwa kwa siku 90 kujishughulisha na masuala ya soka wakati akichunguzwa kwa kashfa za rushwa , alilazwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa afya lakini sasa imeelezwa ataendelea kubaki huko.

Mwanamichezo huyo aliyeongoza ulimwengu wa soka kwa miaka 18 mpaka sasa, awali ilidaiwa alikuwa na matatizo ya msongo wa mawazo hivyo ikabidi apate huduma ya matabibu, sasa imebainika ana tatizo la mshituko wa neva.

Awali, mwanasheria wake, Richard Cullen alieleza juu ya uangalizi huo wa madaktari kutarajiwa, lakini akasema alitarajia arejee nyumbani mapema kabla hali kubadilika na kutolewa maelezo tofauti.

Hata hivyo, watu wake wa karibu wameeleza hali yake si mbaya na anatarajiwa kurejea katika hali ya kawaida japokuwa atabaki hospitalini hadi mapema wiki ijayo.

Msaidizi wake, Walter Gagg, amesema kwamba bosi huyo anatarajiwa kuwa mwenyeji wa hafla ya kukabidhi tuzo ya Mwanasoka Bora hapo Januari 11 mwakani.