Mchezaji ‘aliyechokozwa’ na Costa apewa marashi

Stoke Haki miliki ya picha Getty
Image caption Stoke walizidisha masaibu ya Chelsea kwa kuwalaza 1-0 wikendi

Mchezaji wa Stoke City Ryan Shawcross ameahidiwa manukato ya kumtosha mwaka mmoja baada ya mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa kuonekana kutofurahishwa na harufu ya mwili wake.

Wawili hao walijibizana baada ya kukabiliana wakati wa mechi hiyo ambayo Stoke walishinda 1-0 Jumamosi iliyopita.

Costa alionekana kunusa makwapa yake mwenyewe na kisha kumuelekezea kidole Shawcross kabla ya kujishika pua.

"Tumehakikisha Ryan Shawcross anajipaka marashi yake jioni hii," mkewe difenda huyo wa umri wa miaka 28, Kath aliandika kwenye Twitter baada ya mechi hiyo.

Haki miliki ya picha Getty Images

Shawcross alijiunga na meneja wa klabu hiyo Mark Hughes katika mkutano wa mashabiki wa Stoke ambako alikabidhiwa marashi hayo ya kumtosha mwaka mmoja.

"Costa alipokuwa akiniangazia badala ya kuangazia mechi, sisi tulijishindia mechi,” Shawcross aliambia mkutano huo.

"Yeye ni mchezaji nyota sana na nina furaha kwamba nilimnyamazisha.”