Wasifu wa Aubameyang

Huwezi kusikiliza tena

Mshambuliaji wa Gabon na Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang amekuwa na mwaka wenye mafanikio, akiwa amefunga magoli mengi na kuweka rekodi mpya ya ufungaji Ujerumani.

Msimu wa Bundesliga ulianza mwaka 1963 na kuchipuza wafungaji mabao matata kama vile Gerd Müller, Jupp Heynckes na Karl-Heinz Rummenigge, inahitaji kipaji cha kipekee kuweka rekodi katika ligi hiyo ya ujerumani.

Lakini Mgabon huyu alifanya hivyo, akifunga katika mechi nane za mwanzo za ligi za msimu. Akiipita rekodi ya awali kwa michezo miwili.

Alipofunga katika mechi ambayo walicharazwa 5-1 na Bayern Munich mwanzoni mwa mwezi Oktoba, kijana huyo mwenye miaka 26 aliingia katika vitabu vya kumbukumbu kwa sababu nyingine.

Kwa kuwa alikuwa amefunga katika mechi mbili za mwisho za mwaka 2014-15, alikuwa pia amefunga mabao mfululizo katika mechi 10 za Bundesliga ikiwa ni rekodi ambayo mtu pekee aliyekuwa ameifikia ni Klaus Allofs miaka 30 iliyopita.

“Babangu (mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Gabon) aliniambia kuwa unaweza kufunga katika kila mechi ukitaka,” Aubameyang aliiambia BBC Sport.

“Lakini unahitaji umakini wa hali ya juu kabisa na hilo ndilo ninalolifanyia kazi.”

Baada ya mechi moja ambayo hakufunga (ingawa alitoa usaidizi mara mbili) Mgabon huyu wa kwanza kucheza katika ligi kuu ya Ujerumani alifanya mambo kupitia kile yeye mwenyewe anachokiita...tukio muhimu zaidi kwake mwaka huu.

Katika mechi mbili zilizofuata katika Bundesliga na Europa League alifunga mabao matatu matatu yaani hat-tricks mfululizo.

Baada ya kuongeza ufasaha wa kufunga kwenye kasi yake, ‘Auba’ alifunga mabao 20 katika mechi 17 za kwanza alizochezea Dortmund msimu 2015-16.

Msimu wa 2014-15 Dortmund walimaliza katika nafasi ya 7 baada ya mwanzo mbaya lakini Aubameyang ndiye aliyeng’aa zaidi. Winga huyo aliyebadilika kuwa mshambuliaji alimaliza akiwa kuwa mfungaji bora wa klabu hiyo akiwa na magoli 16 ya ligi.

Pia alifunga matano katika DFB Pokal msimu uliopita, ikiwemo katika robo fainali, nusu fainali dhidi ya Bayern na fainali yenyewe waliposhindwa na Wolfsburg.

Kwa hivyo haikuwa ajabu pale Dortmund waliposema kwamba Aubameyang, waliyemnunua kutoka St Etienne ya Ufaransa 2013, alikuwa akimezewa mate na klabu kadha kuu za Ulaya

Ingawa kiwango chake cha uchezaji akichezea klabu kimevutia sana, Aubameyang bila shaka hawezi akataka kukumbuka fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika kwani hawakufana. Hata hivyo alifunga moja kati ya magoli mawili yaliyofungwa na Gabon dimba hilo nchini Equatorial Guinea.

Aubameyang, mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Milan na timu ya vijana ya Ufaransa, ameingia katika orodha ya wanaowania tuzo ya mwanakandanda bora wa mwaka wa BBC kwa mwaka wa tatu mtawalia.

--------------------------------------------------------------------------------------------------

UCHAMBUZI WA MTAALAMU - John Bennett, BBC World Service

“Ana kasi lakini hawezi kufunga,” wakosoaji walizoea kusema kumhusu Pierre-Emerick Aubameyang lakini mwaka huu amewathibitishia uwezo wake.

Kumekuwepo na vipindi vya ubora kama vile kufuatiliza hat-tricks, lakini ni ule uthabiti wake ndiyo ambao umemfikisha katika hatua ya juu zaidi. Msimu huu ni Robert Lewandwoski wa Bayern Munich pekee anayeweza kushindana naye.

Zaidi ni kuwa Aubameyang amefanya yote haya akiwa na tabasamu katika uso wake. Ni wangapi wanaweza kusahau kusherehekea kwake kama Batman na Robin msimu uliopita? Lakini usidanganyike, kwa sababu Aubameyang amefanya kazi kwa bidii kuubadili uwezo wake kuwa magoli. Alisikiliza waliomkosoa na sasa anafurahia kuwaona wakibadilisha wimbo wao.

Hakuna mchezaji mwingine wa Afrika anayeweza kufananisha uthabiti wa Aubameyang kwa mwaka huu, kwa hivyo yeye ndiye chaguo langu, na jambo muhimu zaidi ni kwamba nadhani huu ndio mwanzo tu kwake.

Walioshinda Tuzo ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka kwa miaka iliyotangulia ni:

Yacine Brahimi (2014);

Yaya Touré (2013);

Christopher Katongo (2012);

André Ayew (2011);

Asamoah Gyan (2010).