Wenger ataka wachezaji wapimwe vizuri

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wenger

Mkufunzi wa Arsenal Arsene Wenger anataka vipimo bora vya dawa za kusisimua misuli kuchukuliwa mara kwa mara miongoni mwa wachezaji wa soka.

Shirikisho la soka nchini Uingereza limemtaka Wenger kuelezea matamshi aliyotoa kuhusu vipimo vya dawa za kusisimu misuli katika mahojiano na gazeti la Ufaransa la L'Equipe.

Raia huyo wa Ufaransa alisema:Niko tayari kwa mazungumzo na FA,''kwa kweli ningependa vipimo bora zaidi kufanywa kwa kuwa vile vinavyofanywa ni vya juu juu''.

''Tunahitajika kukabiliana na swala hili''.

Kiungo wa kati wa timu ya Dinamo Zagreb Arijan Ademi alipatikana na dawa za kusisimua misuli kufuatia ushindi wa timu hiyo dhidi ya Arsenal katika mashindano ya kombe la vilabu bingwa Ulaya.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wachezaji wa Arsenal

Akizungumza kabla ya mechi ya wikendi dhidi ya West Brom,Wenger alisema kwamba ni makosa kudhani kwamba soka haina matatizo kama hayo ikilinganishwa na michezo mingine.

Amesema:''Unaona swala la dawa hizi limeingia katika riadha,tuna tatizo kama hilo katika mashindano ya baiskeli na kufikiri kwamba sisi katika soka hatuwezi kuathiriwa kwa kuwa ni wachezaji soka ni makosa makubwa''.