Katongo aliinua hadhi ya soka ya Zambia

Image caption Katongo aliongoza Zambia kutwaa ubingwa wa Afrika

Christopher Katongo alipokabidhiwa Tuzo ya BBC ya Mwakandanda Bora wa Afrika wa mwaka 2012, mashabiki wa soka nchini Zambia walipata sababu ya kufurahia kuona mmoja wao akiwa kileleni Afrika kwa mara nyingine.

Rais wa sasa wa FA ya Zambia Kalusha Bwalya ndiye pekee aliyewahi kushinda tuzo kuu barani Afrika.

Mwanasoka huyo mwenye kipaji cha kipekee cha soka, na aliyekuwa akitumia mguu wake wa kushoto, alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 1998 ya shirikisho la soka la bara Afrikaa CAF.

Kwa miongo miwili iliyofuata, hakujakuwa na mwanasoka mwingine kutoka Zambia aliyefikia kiwango cha uhodari wake na pia mafanikio yake katika soka.

Hivyo basi, wakati timu ya taifa ya soka Zambia ilinyakua ubingwa wa Afrika mwaka wa 2012, na nahodha wakati huo Christopher Katongo kunyakua tuzo ya mwanasoka bora wa BBC, taifa hilo lilisherehekea kwa furaha.

Mashabiki sana sana walifurahishwa na mafanikio ya Katongo, kwani alitia bidii kusaidia timu yake, na pia akajitoa kwa lengo la kuzoa sifa kwa taifa na pia kwake binafsi kwa zaidi ya miongo miwili.

Wadadisi wengi, mwandishi wa michezo wa BBC Kennedy Gondwe akiwemo, waliamini tuzo ya BBC ilikuwa tu ya kwanza katika kazi yake ya uchezaji soka kwa mtu jasiri, aliyeshirikisha ukwasi wake wa soka na kuwa mwanajeshi.

Mafanikio yake uwanjani pia yalionekana katika kazi yake ya uanajeshi kwani pia alipandishwa cheo.

Wakati wanajeshi wenzake walikuwa wakisherehekea mafanikio yake na kumvulia vilemba, wananchi wenzake walimtizama kwa heshima za juu sana, wakijua fika mafanikio aliyoletea taifa lao.

"Tuzo ya BBC ya mchezaji bora wa mwaka iliinua viwango vya soka hapa Zambia," Mwanahabari wa michezo Ponga Liwewe aliiambia BBC.

"Baada ya miaka mingi ya viwango vya soka kudorora hapa Zambia, tuzo hiyo iliwapa msukumo wachezaji wa Zambia wa kushindana na mataifa bora barani Africa. Katongo ni kama aliokoa soka ya Zambia peke yake."

Katika michuano ya 2006 na 2008 ya kuwania ubingwa wa Afrika, ambayo Katongo alishiriki kwa mara ya kwanza, Zambia ilibanduliwa katika hatua za mapema.

Lakini kwa miaka miwili iliyofuata, Katongo alianza kuleta mabadiliko, na Zambia ikafaulu kuingia robo fainali za kwanza baada ya miaka 14.

Yaliyofuata ni maonyesho yake ya kufana katika fainali za mwaka 2012 zilizokuwa zikifanyika nchini Gabon na Equatorial Guinea.

Umahiri alioonyesha katika dimba hilo ulimaanisha kuwa Katongo - aliyekuwa mfano mwema kwa wenzake kutokana na bidii yake ya kuigwa - angekuwa mchezaji wa kwanza kutoka Zambia kuibuka mchezaji bora wa michuano hiyo ya mataifa bingwa.

Alitia wavuni mabao matatu kwenye fainali, na kuwa kileleni cha ufungaji mabao katika dimba hilo.

Alifunga mabao mawili katika hatua ya makundi, ikiwemo bao moja lililoihakikishia Zambia nafasi katika hatua ya mchujo, na baadaye kufunga matatu dhidi ya Sudan kwenye robo fainali.

Wakati fainali ziliwadia na Ivory Coast waliopigiwa upatu kutwaa ushindi kukosa nguvu za kufunga bao lolote, Katongo aliisadia timu yake kwenye mikwaju ya penalti ya kuamua mshindi iliyofuata, na Zambia ikatwaa ushindi wa kushtusha kwenye historia ya dimba hilo.

Baadaye, sifa na uwezo wake wa kuongoza zilipongezwa kama vigezo muhimu vilivyoifanya Zambia kutia fora.

Raia wa Zambia walifurahia sana wakati Katongo, ambaye alipewa jina la msimbo "Tsunami" - kutokana na ufungaji wake wa mabao alipokuwa akiichezea klabu ya Green Buffalloes alituzwa tuzo ambayo awali ilitwaliwa na wanasoka walioheshimika sana barani Afrika akiwemo Didier Drogba wa Ivory Coast, Andre Ayiew wa Ghana na Jay Jay Okocha wa Nigeria.

"Ulikuwa wakati wa ajabu,” alisema kocha wa awali wa Chipolopolo Patrick Phiri, aliyeshuhudia hafla ya kutoa tuzo ya BBC ya mwanahabari bora barani Africa. "Iliinua Zambia kileleni mwa Africa, hususan kwa sababu alikuwa mwansoka wa kwanza kupokea tuzo hiyo inayoheshimika sana ya BBC"

Katongo mwenyewe alikumbwa na msisimiko mkubwa.

"Hili ni tukio ambalo sitawahi kulisahau maishani mwangu,” Katongo alisema punde tu baada ya kupokea tuzo hiyo.

"Kuwa miongoni mwa wachezaji maarufu waliowahi kushinda tuzo hii ni jambo lisilo la kusadikika". Katongo alisema baada ya kuwapiku Toure, Drogba, Demba Ba wa Senegal na Younes Belhanda wa Morocco.

Kwa sasa Katongo ana umri wa miaka 33, anaelekea kustaafu.

Na baada ya muda mrefu wa kushiriki soka ughaibuni, amerejea kwenye klabu ya Green Buffaloes ambako mafanikio yake yangali yanatambuliwa na mashabiki, ambao mara kwa mara husimama kwa heshima na kumpigia makofi.

Je, Wajua?

Mwaka wa 1994, timu yote ya Zambia ilishinda tuzo ya BBC ya mchezaji bora wa mwaka. Tuzo hiyo ilitolewa baada ya timu hiyo kufika fainali la dimba la kombe la mataifa bingwa Afrika, mafanikio ya kipekee ikikumbukwa kuwa ajali ya ndege ilotokea mwaka 1993 iliuwa wachezaji wao 18 wa timu ya taifa.