Afisi za riadha Kenya zimefungwa siku ya pili

Image caption Afisi za riadha Kenya zimefungwa siku ya pili

Wanariadha wanaendelea kuzingira makao makuu ya shirikisho la riadha la Kenya AK kwa siku ya pili mfululizo kufuatia madai ya kukithiri kwa ufisadi afisini humo.

Hatua yao ilichochewa na ripoti iliyochapishwa juma lililopita iliyodai naibu mwenyekiti wa AK, David Okeyo na maafisa wengine wakuu walihojiwa na maafisa wa kupambana na ufisadi nchini Kenya kufuatia tuhuma za kufyonza takriban dola laki $750,000, kutoka kwa kampuni ya kutengeneza bidhaa za michezo ya Nike.

Okeyo amekana madai hayo dhidi yake.

Kwa siku ya pili mfululizo maafisa wa shirikisho hilo la AK hawakuweza kuingia afisini mwao.

Wakiwa wamebeba mabango ya kukashifu uongozi duni na ufisadi uliokithiri afisini humo wanariadha hao wamefunga lango kuu la afisi hiyo iliyoko karibu na uwanja wa kitaifa wa Nyayo.

Image caption Viongozi wao Wesley Korir na Wilson Kipsang waliwahutubia baada ya kufanya mkutano wa faragha na waziri wa michezo nchini Kenya Hassan Wario.

Viongozi wao Wesley Korir na Wilson Kipsang waliwahutubia baada ya kufanya mkutano wa faragha na waziri wa michezo nchini Kenya Hassan Wario.

Awali mwenyekiti wa shirikisho la riadha alimuambia mwandishi wa BBC mjini Nairobi John Nene kuwa ni ''upuzi mtupu wanachokifanya wanariadha hao nje ya afisi za AK kwani wanariadha mahiri wote wanajiandaa kwa msimu ujao wala sio kukita kambi katika makao makuu ya ya Riadha.''

Kiplagat alisema iwapo muungano wa wanariadha hao wa PAAK wanaushahidi wowowte utakaothibitisha kuwa mamilioni ya fedha za ufadhili wa riadha umefujwa wauwasilishe kwa vyombo vya usalama nchini Kenya.

''Kama wanania ya kuwania uchaguzi basi wasubiri hadi uchaguzi utangazwe rasmi''

'Ninaendelea kuwasiliana na maafisa wa usalama na wakati wowote huo mzozo utatatuliwa mara moja'' alifoka Kiplagat.

Image caption wanariadha hao wanailaumu shirikisho hilo la Athletics Kenya kwa kupokea hongo kutoka kwa mawakala Wanaoshukiwa kuwashawishi wanariadha nchini humo kutumia madawa ya kutitimua misuli yaliyopigwa marufuku duniani.

Vilevile wanariadha hao wanailaumu shirikisho hilo la Athletics Kenya kwa kupokea hongo kutoka kwa mawakala wanaoshukiwa kuwashawishi wanariadha nchini humo kutumia madawa ya kutitimua misuli yaliyopigwa marufuku duniani. Hatahivyo hawajatoa ushahidi wowote kuhusu madai hayo.

Kenya ni moja ya mataifa yaliyotajwa kuwa na tatizo sugu la utumiaji wa dawa hizo za kuongeza nguvu mwilini na shirikisho la kupambana na matumizi ya dawa hizo duniani WADA.

Afisa aliyeongoza uchunguzi wa shirikisho la riadha duniani Dick Pound alishauri WADA iangazie kurunzi yake kwenye afisi za shirikisho la riadha la Kenya baada ya kuitimua Urusi.

Wanariadha hao wanadai kuwa maafisa wa AK wamekuwa wabinafsi sana na sasa wanatishia posho lao.

Kundi hilo la wanariadha linawataka waondoke afisini na pahala pao kuchukuliwa na wanariadha wa zamani