Maafisa wakuu wa riadha Kenya wapigwa marufuku

Image caption Wanariadha wanawalaumu maafisa hao kwa kuhujumu vita dhidi ya madawa haramu ya kuongeza nguvu mwilini

Shirikisho la riadha duniani IAAF imewapiga marufuku kwa muda viongozi watatu wa shirikisho la riadha la Kenya.

Kamati ya maadili ya IAAF imewapiga marufuku ya siku 180 kwa kuhujumu vita dhidi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini.

Waliopigwa marufuku ni rais wa shirikishio hilo Isaiah Kiplagat, naibu wake David Okeyo, na aliyekuwa mweka hazina wa AK Joseph Kinyua.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Licha ya Kenya kutawala duniani katika riadha haina mpango madhubuti wa kupambana na dawa haramu

Kinyua vilevile alikuwa kiongozi wa ujumbe wa Kenya katika mashindano ya riadha mwaka huu 2015.

Aidha Watatu hao wanadaiwa kupunja fedha zilizokusudiwa kufadhili ustawi wa michezo udhamini wa kampuni ya kutengeza bidhaa za michezo kutoka Marekani Nike.

Yamkini dola laki 750 zilipunjwa.

Image caption Isaiah Kiplagat, naibu wake David Okeyo, na aliyekuwa mweka hazina wa AK Joseph Kinyua wamepigwa marufuku ya siku 180

Maafisa hao wamekanusha madai yote dhidi yao.

Ni majuzi ambapo kundi la wanariadha lilifanya maandamano makubwa na kujifungia katika makao makuu ya shirikisho la riadha nchini Kenya ya Riadha House wakitaka maafisa hao wakuu kuondoka madarakani.

Haki miliki ya picha b
Image caption Wakenya zaidi ya 40 wamepigwa marufuku kwa kutumia madawa ya kuongeza nguvu mwilini

Kundi hilo chini ya muungano wa wanariadha PAAK linaloongozwa na Wesley Korir na Wilson Kipsang lilitaka mabadiliko yafanyike mara moja ilikuwezesha shirikisho hilo kupambana dhidi ya matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini.

Viongozi hao yamkini walisema hayo baada ya kufanya mkutano wa faragha na waziri wa michezo nchini Kenya Hassan Wario.

Kwa mujibu wa kamati ya maadili ya IAAF, Kiplagat anatuhumiwa kutunukiwa zawadi ya magari mawili kutoka kwa shirikisho la riadha la Qatar.

Kamati hiyo inapeleleza zawadi hiyo huku ikifahamu kuwa Qatar hivi majuzi tu ilishinda zabuni ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya ubingwa wa dunia mwaka wa 2019.