Kigogo wa Man Utd afanywa kocha wa Valencia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gary Neville atasalia kwenye benchi la wakufunzi wa England

Difenda wa zamani wa Manchester United na Uingereza Gary Neville ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa klabu ya Valencia hadi mwisho wa msimu.

Neville, 40, atachukua majukumu kamili Jumapili, na atasalia kwenye benchi la wakufunzi la Uingereza.

Peter Lim, mmiliki wa Valencia anayetoka Singapore, ana hisa katika klabu ya Salford City, ambayo Neville ni mmiliki mwenza.

Kakake Neville, Phil, aliyejiunga na klabu hiyo ya Uhispania kama meneja msaidizi Julai atasalia kwenye benchi la wakufunzi.

"Nimefurahia sana kupewa fursa hii,” amesema Neville.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Neville atasimamia mechi yake ya kwanza Valencia Jumatano

“Valencia ni klabu kubwa – na najua kujitolea kwa mashabiki wake, kutoka kwa wakati wangu nikiwa mchezaji.”

Mechi ya Jumatano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Lyon itakuwa ya kwanza kwa Neville akiwa kwenye usukani.

Neville amechukua nafasi ya Nuno Espirito Santo, aliyejiuzulu baada ya Valencia kuchapwa 1-0 ugenini Sevilla. Klabu hiyo kwa sasa imo nambari tisa ligi ya Uhispania.