Rwanda na Uganda zatinga fainali Cecafa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rwanda itakuwa mwenyeji wa CHAN mwaka 2016

Rwanda na Uganda zimefika fainali ya kombe la Cecafa 2015 baada ya kuandikisha ushindi nusufainali kupitia mikwaju ya penalti.

Rwanda walitinga fainali baada ya kucharaza Sudan 4-2, nao Uganda wakawalaza wenyeji wa michuano hiyo Ethiopia 5-3. Fainali itachezwa Jumamosi, sawa na mechi ya kuamua mshindi wa tatu kati ya Ethiopia na Sudan.

Sudan walisalia wachezaji kumi uwanjani baada ya Bakri Osman Idriss kufukuzwa uwanjani dakika ya 10 ya mechi lakini waliweza kujikinga dhidi ya Rwanda na hata kulazimisha mechi kwenda muda wa ziada.

Atahir El Tahir kisha aliwapa Sudan bao la uongozi dakika ya 100 lakini Rwanda wakasawazisha kupitia Jean Baptiste Mugiranza dakika 10 baadaye.

Rwanda nao walikamilisha kujikwamua kwao kwa kushinda kwa mikwaju 4-2 kwenye matuta, El Tahir na Mazin Elfalah Ahmed wakishindwa kufunga mikwaju yao.

Kocha wa Rwanda Johnny McKinstry alisema: "Timu yangu changa imefanyia fahari taifa kwa kufika fainali.”

Raia huyo wa Ireland Kaskazini pia anatumia michuano hiyo kuandaa timu yake kwa michuano ya Kombe la Taifa Bingwa Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani (CHAN) 2016 ambayo Rwanda itakuwa mwenyeji.

Uganda, mabingwa mara 13 wa Cecafa, walitoka sare tasa na Ethiopia, hata baada ya muda wa ziada.

Kipa wa Cranes Ismail Watenga alikomboa mkwaju wa kwanza uliopigwa na Gatoch Panom na timu yake ikakwamilia uongozi kwenye matuta hadi mwisho.

Nahodha wao Farouk Miya ndiye aliyewafungia penalti ya ushindi.

Uganda watakapokuwa wakisaka ubingwa mara ya 14, Rwanda watakuwa wakisaka kombe lao la pili, mara yao pekee kutwaa ubingwa ikiwa 1999.