Man Utd kucheza Europa League

Naldo Haki miliki ya picha Getty
Image caption Naldo alifungia Wolfsburg mabao mawili

Manchester United wameondolewa kutoka kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kushindwa na klabu ya Wolfsburg kutoka Ujerumani Jumanne usiku.

Vijana hao wa Old Trafford waliondoka Ujerumani na kichapo cha 3-2, na kumaliza wakiwa nambari tatu katika kundi lao hii ina maana kwamba sasa watacheza Europa League.

Kwenye kundi lao, Vfl Wolfsburg walimaliza kileleni wakifuatwa na PSV Eindhoven. CSKA Moscow walishika mkia.

Red Devils walikuwa wameanza vyema Anthony Martial alipowafungia baada ya kupata pasi kutoka kwa Juan Mata.

Lakini wenyeji wao Wolfsburg walikomboa dakika tatu baadaye kupitia Naldo kisha wakajiweka kifua mbele kupitia Vieirinha.

United walidhani wangesonga mbele baada ya Josuha Guilavogui kujifunga lakini mwishowe wakajipata wametumwa Europa League baada ya Naldo kufunga kwa kichwa dakika za mwisho.

Vijana hao wa Louis van Gaal walijuwa wangefuzu kwa hatua ya 16 bora iwapo wangelaza Wolfsburg, au wafikie matokeo ya PSV Eindhoven waliokuwa wakicheza dhidi ya CSKA Moscow.

Matumaini yalikuwepo baada ya CSKA kuongoza 1-0 ugenini Eindhoven lakini baadaye PSV waliibuka na ushindi wa 2-1.

Matokeo kamili ya mechi zilizochezwa Jumanne usiku:

  • Paris St Germain 2 - 0 Shakhtar Donetsk
  • Real Madrid 8 - 0 Malmö FF
  • VfL Wolfsburg 3 - 2 Man Utd
  • Manchester City 4 - 2 B Monchengladbach
  • PSV Eindhoven 2 - 1 CSKA Moscow
  • Benfica 1 - 2 Atl Madrid
  • Galatasaray 1 - 1 FC Astana
  • Sevilla 1 - 0 Juventus