Carneiro kuendelea na kesi dhidi ya Chelsea

Carniero Haki miliki ya picha AFP
Image caption Carniero aliondoka Chelsea mwezi Septemba

Daktari wa zamani wa Chelsea Eva Carneiro anapanga kuendeleza na kesi dhidi ya Chelsea na aliyekuwa meneja Jose Mourinho.

Carneiro ameishtaki Chelsea kwa kumfuta kazi na kukiuka masharti ya mkataba wa kazi. Kuna pia kesi tofauti dhidi ya Mourinho ya madai ya ubaguzi.

Kabla ya kikao cha kwanza cha kesi kusikizwa 6 Januari, Chelsea waliwasilisha taarifa ya kujitetea muda mfupi kabla ya wakati wa mwisho Alhamisi.

Mourinho alifutwa kazi Alhamisi.

Tarehe kamili ya kikao cha kusikiza madai hayo itapangwa mwaka ujao, na Mourinho na maafisa wa Chelsea watatakiwa kutoa ushahidi binafsi.

Kwenye madai yake Carniero anataka pia arejeshwe kazini, jambo linaloibua uwezekano wake kurejea Stamford Bridge. Hata hivyo, klabu hiyo haitalazimishwa kumrejesha kazini.

Aliondoka klabu hiyo Septemba baada ya kushushwa cheo siku chache baada ya kukosolewa na Mourinho kwa kuingia uwanjani kumtibu Eden Hazard wakati wa mechi ambayo walitoka sare 2-2 na Swansea.

Mourinho alishutumiwa vikali kwa kumkosoa daktari huyo lakini aliondolewa mashtaka ya kutumia lugha ya kibaguzi na Shirikisho la Soka la Uingereza.