Mameneja washangazwa na kufutwa kwa Mourinho

Mourinho Haki miliki ya picha AFP Getty Images
Image caption Mourinho alifutwa kazi Alhamisi

Mameneja wa klabu za Ligi Kuu ya Uingereza wameeleza kushangazwa kwao na hatua ya Chelsea kumfuta kazi meneja Jose Mourinho.

Jose Mourinho, 52, alifutwa Alhamisi miezi saba baada ya kuwaongoza kushinda Ligi ya Premia.

Chelsea kwa sasa wamo alama moja tu juu ya eneo la kushushwa daraja baada ya kushindwa mechi tisa kati ya 16 walizocheza ligini msimu huu.

Hivi ndivyo walivyosema mameneja wenzake EPL:

Louis van Gaal - Manchester United:

Haki miliki ya picha Reuters

"Nimeshangaa sana, si jambo nililolitarajia. Ni meneja mzuri sana na mwenye rekodi ambayo hakuna mwingine anayeifikia katika ulimwengu wa soka, lakini hili linawezekana. Siwezi kusema ni nini kilikuwa kinaendelea Chelsea, lakini nimeshangaa.”

Manuel Pellegrini - Manchester City:

“Ligi ya Premia imempoteza meneja muhimu sana. Labda meneja ninayetofautiana sana naye katika mengi, lakini ukifikiria vingine – yeye si adui wangu.

"Nafikiri Ligi ya Premia itamkosa. Mimi, sina haja kumkosa mtu fulani, lakini ningependelea Ligi ya Premia ikiwa na Mourinho kushinda ikiwa bila Mourinho.”

Alex Neil - Norwich:

"Nguvu ambazo wachezaji wanazo zimeongezeka sana. Kilichofanyika Chelsea kinaonyesha mchezo ulivyo sasa. Klabu zina wachezaji ‘bidhaa’ wa thamani ya mamilioni. Ni rahisi kutimua mmoja kuliko zaidi ya 20.”

Sam Allardyce – Sunderland

“Habari hizi zimenishangaza. Nakubali kwamba kama mameneja hatuwezi kuendelea daima iwapo matokeo hayaridhishi, lakini sikudhani hili lingetokea wiki hii – au kabla ya kipindi cha mechi nyingi zaidi.”

West Ham- Slaven Bilic:

"Ninaweza tu kusema kuhusu Mourinho kwamba bila shaka nimeshangazwa sana. Unapokuwa bora zaidi, kuna wengi wanaotaka uporomoke. Hakuna ajuaye kama Jose angeweza kubadilisha hali. Ninaamini angeliweza. Hii si mara ya kwanza hili kutendekea timu kubwa. Jambo sawa lilifanyikia Borussia Dortmund [chini ya meneja wa sasa wa Liverpool Jurgen Klopp] msimu uliopita.

"Kuondoka kwa Mourinho kunaonyesha hakuna aliye salama.”

Tony Pulis - West Brom:

Haki miliki ya picha Getty

"Ndiye meneja bora zaidi ligini kwa sasa. Timu zetu zimekabiliana mara nyingi. Amekuwa mwema kwangu. Nimesikitika.”

Bournemouth's Eddie Howe:

"Nilishangazwa na kusikitika sana niliposikia kumhusu Jose Mourinho. Ni tukio la kuhuzunisha mtu anapopoteza kazi.”