Telkom Kenya ndio mabingwa wa Afrika wa magongo

Image caption Telkom Kenya ndio mabingwa wa Afrika wa magongo

Timu ya Telkom ya Kenya na Eastern Company ya Misri zimetwaa ubingwa katika mashindano ya magongo ya klabu bingwa Afrika yaliyomalizika leo hii mjini Lusaka, Zambia.

Telkom imeshinda Ghana Police kwa mabao 3-2 ya penalti baada ya sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida.

Wakati huo huo Eastern Company ikishinda wenzao kutoka Misri na bingwa mtetezi Sharkia kwa mabao 2-1.

Mechi ya Telkom haikumalikizika jana ikabidi ichezwe mapema leo kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mjini Lusaka.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama cha mchezo wa magongo nchini Kenya, Nashon Randiek, mechi hiyo ilianza saa kumi na mbili za asubuhi kuwezesha timu ziondoke kwa muda uliopangwa.

Telkom ndio waliona lango la mwanzo kunako dakika ya 53 kupitia kwa Jacqueline Wangechi na dakika tatu baadae Linda Sasu akaifungia Ghana Police bao la kusawazisha...

Wafungaji wa penalti wa Telkom walikua ni Teresa Juma, Barbara Simiyu na Adrey Omaido huku Serwa Boakye na nahodha Rejoice Noi wakiifungia Ghana Police..

Katika mechi ya wanaume Eastern Company waliongoza kwa bao 1-0 kufikia muda wa mapumziko.

Mfungaji akiwa ni Fadl Gamal dakika ya 10 kisha Ahmed Hakim akaongeza la pili dakika ya 67 naye Hosam Gorban akaipa Sharkia bao lao moja dakika ya 70..

Hii ni mara ya 8, na ya nne mfululizo Telkom inaibuka mshindi katika mashindano haya ya klabu bingwa Afrika kwa wanawake.

Wameshinda taji hilo tangu mwaka wa 2012, na mwaka jana waliposhinda kwa mara ya tatu mfululizo kombe likawa ni lao kabisa...hili ambalo wameshinda leo hii mjini Lusaka ni jipya..